Makumi ya vijana katika kaunti ya Siaya, eneobunge la Bondo wameandamana na jeneza kwenda ofisi ya mbunge wao, Gideon Ochanda kuashiria kifo chao baada ya mbunge huyo kupiga kura ya kuunga mkono mswada wa fedha wa 2024.
Katika video ambazo zimeenezwa katika mitandao ya kijamii, vijana hao walionekana wamebeba jeneza mabegani wakiandamana kuimba nyimbo za kumkashifu Ochanda.
Ochanda, ambaye ni mbunge wa mrengo wa Azimio ambao walikuwa wanaupinga mswada huo aliwashangaza wengi baada ya kupiga kura kuunga mkono mswada huo.
Jeneza hilo lilikuwa limepakwa rangi ya maneno ya kumkashifu Ochanda wakimtaja kama mfu wa ‘Sugoi’ – nyumbani kwa rais William Ruto.
Katika kura hiyo ya kusomwa kwa mara ya pili kwa mswada huo, wabunge 204 walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo huku wabunge 115 wakipiga kura ya kuukataa.
Idadi kubwa ya wabunge waliopiga kura ya kuunga mkono walikuwa kutoka mrengo wa serikali wa Kenya Kwanza.
Wengi waliopiga kura ya kuupinga walikuwa kutoka mrengo wa upinzani wa Azimio.
Tazama video hii jinsi vijana hao waliandamana wakiwa na jeneza.