DP Rigathi Gachagua azungumza baada ya kumzika dadake mkubwa

Gachagua alimuomboleza dadake kama mwanamke wa kipekee ambaye ameacha alama kubwa katika jamii.

Muhtasari

• Jumatano dada mkubwa wa naibu rais, marehemu Leah Wangari Muriuki alizikwa katika eneo la Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

•DP aliwashukuru watu wote ikiwa ni pamoja na viongozi ambao wameonyesha sapoti kwa familia katika wakati huu mgumu.

wakiweka shada la maua wakati wa mazishi ya dadake Naibu Rais huko Nanyuki Julai 3, 2024.
Naibu Rais Rigathi Gachagua akiwa na mkewe Mchungaji Dorcas Rigathi wakiweka shada la maua wakati wa mazishi ya dadake Naibu Rais huko Nanyuki Julai 3, 2024.
Image: DPCS

Siku ya Jumatano, Julai 3, dada mkubwa wa naibu rais Rigathi Gachagua, marehemu Leah Wangari Muriuki alizikwa katika eneo la Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Marehemu Leah Wangari aliaga dunia takriban wiki moja iliyopita na naibu wa rais alikuwa ameeleza masikitiko yake kuhusu hali ya kusikitisha iliyoikumba familia yao.

Baada ya kumzika mkubwa huyo wake mnamo Jumatano, Gachagua aliendelea kumuomboleza kama mwanamke wa kipekee ambaye ameacha alama kubwa katika jamii.

“Leo, tumemzika Dada yetu mkubwa Leah Wangari Muriuki, mwanamke muhimu katika jamii.  Mwalimu na mshauri mwenye busara sana, Familia ya Gachagua, Familia ya Gatata na jamii ya Mirera huko Nanyuki watakosa ushauri wake wa busara,” Gachagua aliomboleza kupitia mtandao wa Facebook.

DP aliendelea kuwashukuru watu wote ikiwa ni pamoja na viongozi ambao wameonyesha sapoti kwa familia katika wakati huu mgumu na wale waliohudhuria mazishi.

 “Tunashukuru viongozi, ambao wameomboleza nasi, wakiongozwa na Rais wetu H.E William Samoei Ruto, na Wananchi ndani na bila Kaunti za Laikipia na Nyeri. Tunaomba muendelee kutuombea katika wakati huu mgumu.  Shine on to Glory Leah,” aliandika.

Naibu rais alitangaza kifo cha dadake mkubwa siku chache zilizopita katika chapisho la kihisia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Katika tangazo lake, Gachagua alielezea masikitiko yake na kudokeza jinsi marehemu Leah alivyokuwa muhimu katika familia yao.

“Nimehuzunishwa kupokea habari za kufariki kwa dada yetu mkubwa Leah Wangari Muriuki. Leah amekuwa mama yetu na mkubwa wa familia; ameitunza vyema Familia kubwa ya Gachagua baada ya kifo cha baba yetu na mama zetu wawili,” Gachagua alitangaza kwenye Facebook.

Aliongeza, “Tumesikitishwa sana na kifo cha mkuu wa familia huyu. Pole zangu za dhati kwa mume wake, watoto wake na wajukuu zake. Wiki hii ni ngumu sana kwangu kama kiongozi wa kitaifa na mwanafamilia. Bwana aliponya Taifa na familia zetu.

Naibu rais alimpoteza dadake takriban miaka miwili tu baada ya kifo cha kakake Jack Reriani.