Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema nchi imepoteza takriban Sh6 bilioni kutokana na maandamano ya Gen Z.
"Kwa jumla, nchi imepoteza takriban Sh6 bilioni, kulingana na mamlaka ya ushuru ya Kenya, kutokana na maandamano," alisema.
Mwaura alisema kuna hofu kwamba iwapo maandamano hayo yataendelea, uchumi utaathirika vibaya zaidi.
Aliendelea kwa kusema kuwa serikali haina ugomvi wowote na wanahabari kufuatia kukamatwa kwa mwanahabari Macharia Gaitho.
"Serikali haina ugomvi na wanahabari yule aliyeshikwa aliwachiliwa na polisi kwa utambulisho wa makosa .Tuko tayari kufanya kazi na nyinyi ili mfanye kazi kwa uhuru." Mwaura alisema.
Hata hivyo alisema kuwa serikali inajaribu kwa sana kusikiliza maoni ya wananchi hasa baada ya kuvunja baraza la mawaziri na kutupilia mbali mswada wa fedha wa 2024,kutia sahihi mswada wa IEBC na kupunguza makadirio ya fedha katika ofisi maalum.