Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kusitisha kampeni za kuwania muhula wa pili wa urais na kusema amechukua uamuzi huo ''kwa maslahi ya chama chake na nchi.''
Uamuzi wa Biden kujitoa kwenye mbio za urais umekuja ikiwa imesalia miezi minne pekee kabla ya Wamarekani kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu.
Kwa wiki kadhaa sasa Biden amekuwa akishinikizwa ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho na wanachama wenzake wa chama cha Democrats baada ya kufanya vibaya kwenye mjadala na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump mwishoni wa mwezi Juni.
Katika barua aliyoituma kupitia mitandao yake ya kijamii, Biden amesema imekuwa ni Fahari ya Maisha yake kuhudumu kama rais.
"Japo ilikuwa ni azma yangu kuwania muhula wa pili, naamini itakuwa ni manufaa kwa chama changu na nchi mimi kujiengua na kujielekeza katika kukamilisha majukumu ya Urais kwa kupindi kilichosalia cha muhula wangu.”
Kiongozi huyo ameahidi kulihutubia taifa kuhusu uamuzi wake huo juma lijalo.
Rais Biden pia amemshukuru Makamu wake Kamala Harris, akisema alikuwa “mshirika wa kipekee.”
"Na acha nitoe shukrani zangu za dhati kwa watu wa Marekani kwa imani na uaminifu mlioweka kwangu," taarifa yake iliongeza.
"Ninaamini leo na daima : kwamba hakuna kitu ambacho Amerika haiwezi kufanya, tunapofanya pamoja. Inabidi tukumbuke sisi ni Marekani."
Wiki iliyopita alirudi nyumbani kwake huko Delaware baada ya kugunduliwa na kuwa na virusi vya Covid, lakini alisema Ijumaa alikuwa anatazamia "kurejea kwenye kampeni wiki ijayo".
Hapo awali alisema ni "Mwenyezi Mungu" pekee ndiye anayeweza kumfanya ajiondoe, lakini baadaye akasema angefikiria kujiondoa ikiwa atakuwa na sababu ya kiafya.
Akijibu kwenye jukwaa lake la Truth Social , mgombea Republican Donald Trump alisema kuwa Joe Biden "hakuwa sawa kugombea urais".