Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti amemshauri Rais William Ruto kuchukua muda wake kutathmini na kuchagua watu watakaounda baraza lake la pili la mawaziri.
Akizungumza alipokuwa akihudhuria misa ya Jumapili katika eneo la Athi river, Wavinya aliambia Rais kuwa wakenya wapo makini jinsi atakavyoteua baraza la mawaziri waliosalia.
“Achukue muda, asikurupuke. Anapaswa kuchukua muda kusikiliza Wananchi, na kuchagua watu wanaowataka. Wanaoweza kutumikia wananchi,” Wavinya alisema.
Gavana huyo alidai kuwa ingawa wafanyikazi wa umma hawakosi makosa, Rais ana fursa ya kuwatambua na kuwachagua watu ambao wanaweza kuwafanyia kazi wakenya.
Rais William Ruto aliwateua mawaziri 11 wa baraza la mawaziri kwa serikali yake julai 19. Uteuzi huo ulijiri wiki kadhaa baada ya rais kulifuta baraza lake lote la mawaziri isipokuwa waziri mkuu Musalia Mudavadi.
Taifa bado linasubiri rais Ruto kutaja mawaziri zaidi wa baraza lake la pili la mawaziri.