KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumanne, Julai 23.
Katika taarifa ya Jumatatu jioni, kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanyika kwenye mitambo.
Walisema baadhi ya maeneo ya kaunti saba za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni. Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na Kiambu, Makueni, Nakuru, Uasin Gishu, Kisii, Nyeri, na Murang'a.
Katika kaunti ya Kiambu, sehemu za maeneo ya Thindigua na Muhasibu zitaathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Sehemu za maeneo ya Kiamunyi na Mercy Njeri katika kaunti ya Nakuru zitakosa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi alasiri.
Baadhi ya sehemu za maeneo ya Kamukunji na Block 10 katika kaunti ya Uasin Gishu zitaathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.
Sehemu kadhaa za eneo la Wote katika kaunti ya Makueni zitaathirika kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja alasiri.
Katika kaunti ya Kisii, sehemu za mji wa Kisii zitakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi alasiri.
Baadhi ya sehemu za maeneo ya Kabebero na Kihuri katika kaunti ya Nyeri zitakosa umeme kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Katika kaunti ya Murang'a, wakazi wa maeneo ya Pundamilia na Ndera watashuhudia kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuh na saa kumi na moja alasiri.