logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Alai: Ruto ni mmoja wa wanzilishi wa ODM, akiamua kumpa mtu yeyote wa ODM kazi asizuiwe!

Alai alimpendekeza mbunge maalum John Mbadi katika wadhifa wa waziri wa fedha.

image
na Davis Ojiambo

Habari24 July 2024 - 08:14

Muhtasari


  • • Kwa mujibu wa MCA huyo wa ODM, Ruto kama mmoja wa waasisi wa ODM karibia miaka 20 iliyopita, ana kila haki ya kumteua mtu wa ODM katika baraza lake la mawaziri.
ROBERT ALAI, MCA KILELESHWA

Diwani wa Kileleshwa, Robert Alai amesisitiza kwamba hakuna hatia yeyote ikiwa rais Ruto ataamua kumteua mwanachama yeyote wa ODM katika baraza lake la mawaziri.

Alai kupitia ukurasa wake wa X alisema kwamba wale wanaopinga uteuzi wa wanachama wa ODM Katika baraza la mawaziri la rais Ruto wanafaa kurudisha nyumba kumbukumbu zao na kufahamu kwamba Ruto ni mmoja wa waanzilishi wa chama cha ODM.

Kwa mujibu wa MCA huyo wa ODM, Ruto kama mmoja wa waasisi wa ODM karibia miaka 20 iliyopita, ana kila haki ya kumteua mtu wa ODM katika baraza lake la mawaziri.

Alai alipinga vikali baadhi ya watu katika chama hicho cha upinzani ambao wanatoa vitisho kwa wanachama wao kukataa teuzi serikalini iwapo rais Ruto atapendekeza majina yao kwa madai kwamba teuzi hizo hazitakuwa zimepata Baraka kutoka kwa uongozi wa chama.

Alai akipendekeza mbunge maalum John Mbadi kuwa waziri wa fedha, alisema kuwa Ruto kumpa mtu wa ODM kazi serikalini itakuwa kama kurudisha shukrani kwa chama kilichomuinua katika ulingo wa siasa.

“Ruto ni mmoja wa waanzilishi wa ODM. Iwapo ataamua kuteua ODM yoyote kwa baraza la mawaziri, mvivu yeyote katika chama anayedai kuwa mtendaji wa chama hafai kuzuia uteuzi huo. Ruto atakuwa akisema asante pia kwa ODM kwa kuwa chama kilichomsukuma katika uzito wa uongozi wa kisiasa. Mbunge Mbadi anaweza kuwa CS Fedha!” Alai alisema.

Kauli ya Alai inajiri saa chache baada ya katibu mkuu wa ODM ambaye pia ni seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kutoa barua inayowaonya wanachama dhidi ya kukubali uteuzi wowote serikalini.

Katika barua hiyo, Sifuna alionya kwamba yeyote atakayekubali uteuzi serikalini atakuwa anafanya hivyo kwa msimamo wake binafsi na wala haitokuwa uamuzi na Baraka kutoka kwa viongozi wa chama.

Saa chache baadae, Mbunge wa Homabay mjini Peter Kaluma alimsuta vikali Sifuna kwa barua hiyo akisema kwamba huo si uamuzi ambao waliafikiana katika mkutano mkuu wa chama siku chache zilizopita.

Kaluma alisema kwamba wanaweza anzisha mchakato wa kumbandua Sifuna kutoka wadhifa wa katibu wa chama kwa kile alidai kwamba alichapisha kauli inayokinzana na maamuzi yaliyoafikiwa wakati wa mkutano mkuu wa ODM.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved