Vikosi vya uokoaji kufikia sasa vimeopoa miili ya watu 229 ya watu waliouawa katika maporomoko mawili ya udongo kusini mwa Ethiopia, afisa wa eneo hilo ameiambia BBC.
Maporomoko hayo ya udongo yalitokea Jumapili jioni na Jumatatu asubuhi, baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo la lisiloweza kufikiwa kwa urahisi la milima la ukanda wa Gofa.
Mamlaka ya eneo hilo imesema kuwa utafutaji wa manusura ulikuwa "unaendelea kwa nguvu" lakini "idadi ya vifo bado inaweza kuongezeka".
Picha zilionyesha mamia ya watu wakiwa wamekusanyika kwenye eneo la tukio na wengine wakichimba kwenye matope kutafuta watu waliokwama chini.
Afisa mkuu wa utawala wa eneo la Goza, Dagmawi Ayele, ameiambia BBC kuwa waliofariki ni pamoja na watu wazima na watoto, huku watu 10 waliookolewa wakiwa hai wakipokea matibabu hospitalini.