Ripoti kuhusu athari za mafuriko kwa shule iliyofanywa na jopo kazi la Elimu Bora inaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi 15,000 hawakuendelea na masomo.
Kulingana na utafiti huo, takwimu kutoka shule 60 zilizofanyiwa utafiti zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi ilipungua kutoka 23,530 hadi 21,453 baada ya mafuriko ikiashiria upungufu wa asilimia tisa.
Kiwango cha kurudi kwa wanafunzi wa kike kilipungua kwa takriban asilimia 10, asilimia 11 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum - 40 kati ya 337 ya awali - walikuwa bado hawajarejea.
Makazi yasiyo rasmi ya Mathare ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko mabaya ambayo yalisababisha uharibifu kote nchini kati ya mwezi Aprili na Mei.
Gatuzi hilo dogo liliandikisha kiwango cha juu zaidi cha kuacha shule huku familia 7000 zikiathiriwa vibaya.
“Makazi mengi yasiyo rasmi katika maeneo ya mijini yaliteseka sana; kwa mfano, zaidi ya watu 7,000 walikimbia makazi yao katika makazi yasiyo rasmi ya Mathare jijini Nairobi pekee” inasomeka ripoti hiyo.
Wakati huo huo, shule 62 zilizama huku vyoo 20,000 vikizama au kuharibiwa vibaya na mafuriko na kusababisha hatari kubwa ya kiafya kwa zaidi ya wanafunzi milioni 1.5.
Visa 34 vya ugonjwa wa kipindupindu viliripotiwa katika Kaunti ya Tana River, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka huku watoto wakitarajiwa kurejea shuleni.
Shule nyingi zilizoathiriwa na mvua kubwa na mafuriko katika kaunti hiyo ziliteseka kimsingi kutokana na mifumo duni ya mifereji ya maji. Kwa hiyo, maeneo mengi yalibakia kuzama na mashamba yaliyojaa maji kulingana na utafiti.
Ripoti hiyo, hata hivyo, inaangazia juhudi kubwa za ushirikiano kati ya walimu wakuu, bodi za usimamizi na vyama vya wazazi.
"Ushirikiano huu uliwezesha ujenzi wa miundo ya muda ya kujifunza na kuunda mfumo wa kina wa kukabiliana na maafa. Juhudi za uratibu ziliongozwa na kamishna msaidizi wa kaunti na msimamizi wa kaunti ndogo” kundi hilo linafichua.
Kufikia Mei 10, 2024, Kituo cha Kitaifa cha Operesheni ya Maafa kiliripoti vifo 267, majeruhi 188, na watu 75 waliopotea.
Zaidi ya hayo, watu 281,835 (familia 56,367) walikimbia makazi yao, na karibu watu 380,573 (familia 76,114) waliathiriwa na mvua kubwa na mafuriko yaliyoendelea (Kenya, 2024).
Mafuriko hayo pia yalisababisha hasara ya mifugo zaidi ya 9,973, uharibifu wa ekari 41,562 za mashamba na barabara 61, na uharibifu wa biashara 886, shule 1,967, vyanzo vya maji 1,465, na vituo vya afya 62 katika kaunti 11 kati ya 42 zilizoathiriwa.