logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Baadhi ya viongozi na Gen Z wamshtumu Raila kwa kuungana na serikali

“Rais ameamua kuwa atatawala nchi hii bila Katiba ambayo aliapa kuilinda, kuitetea na kuikuza,” alisema Omtatah

image
na SAMUEL MAINA

Habari25 July 2024 - 07:40

Muhtasari


  • •Wanachama wanne wa Orange Democratic Movement (ODM) walipata mwaliko wa karamu ya Kenya Kwanza, na kupata nafasi nzuri za Baraza la Mawaziri.
  • •"Damu na machozi ya vijana isikupe amani maisha yako yote," alisema aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana

Baadhi ya viongozi na vijana machachari wa kizazi cha Gen Z wamemshutumu aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kwa kutumia maandamano yao dhidi ya serikali kujinufaisha.

Tangazo la Rais Ruto la kuibua baraza jiya la mawaziri lilikuwa kama lilivyotarajiwa huku likizidi kuibua mdahalo mkali baina ya wananchi.

Tangu alipodokeza kuundwa kwa serikali ya mseto, akiibatiza "serikali yenye msingi mpana", Rais William Ruto aliweka wazi kuwa anakaribisha upinzani wa Raila Odinga kushirikiana naye.

Siku ya Jumatano, wanachama wanne wa Orange Democratic Movement (ODM) walipata mwaliko wa karamu ya Kenya Kwanza, na kupata nafasi nzuri za Baraza la Mawaziri.

Ruto alimteua Mwenyekiti wa ODM John Mbadi kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri la Hazina ya Kitaifa, huku Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi akichukua hati ya Nishati na Petroli.

Manaibu wawili wa Raila, Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, pia, walipata viti katika meza inayotamanika kama wateule wa Madini na Vyama vya Ushirika, mtawalia.

Katika siku chache zilizopita, upinzani Azimio la Umoja-One Kenya ulizozana kuhusu kujiunga na serikali ya Ruto huku washirika wengine wakipinga ushirikiano na Ruto.

Vita hivyo vimekuwa vikali ndani ya ODM ambayo imegawanyika kuhusu kujiunga na Kenya Kwanza ili kusaidia kupunguza hali ya kutoridhika iliyoenea kuhusu uendeshaji wa mambo ya serikali.

Tangazo la Rais, ambalo pia lilijumuisha kurudishwa kwa watumishi wa zamani, lilikasirisha  Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, ambao walitilia shaka dhamira yake ya kurekebisha mfumo mbovu ambao unawanyima haki wengi.

"Raila wewe si Raila Odinga BABA tena. Harakati za GENZEE-MILLENNIAL MOVEMENT sasa ni UPINZANI RASMI. Sasa uko kwenye shake yako ya nne -Moi, Kibaki, Uhuru & Ruto - handchequeshake.

Siku zote zimefichwa mbele ya macho. Damu na machozi ya vijana isikupe amani maisha yako yote," alisema aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana

Mwanaharakati Boniface Mwangi aliandika: "Raila Odinga unasema vijana hawa waliuawa ili wewe, na marafiki zako wapate ajira? Walikufa kwa ajili ya Kenya bora, isiyo na uongozi mbaya, ufisadi, ukabila na siasa za kukaguliwa. Hii ni kiwango cha usaliti hakisameheki.Hatutasahau."

Seneta wa Busia Okiya Omtatah alitaja hatua ya upinzani kuingia serikalini kuwa ni ukiukaji wa Katiba, akisema ni kinyume cha vyama vingi.

“Rais ameamua kuwa atatawala nchi hii bila Katiba ambayo aliapa kuilinda, kuitetea na kuikuza,” alisema Omtatah.

Vilevile, aliteta kuwa kuteuliwa kwa wabunge kwenye Baraza la Mawaziri kutaingiza gharama zisizo za lazima kwa mlipa ushuru kutokana na uchaguzi mdogo utakaohitaika kufanyika.

Wakati wa X Space iliyopewa jina la 'Ruto is a joker', wengi walimwaga masikitiko yao katika uteuzi wa Baraza la Mawaziri, wakipendekeza maandamano yazidishwe.

Baadhi walipendekeza kuteuliwa kwa "mgombea wa vuguvugu la maandamano" katika kiti cha ubunge cha Ugunja, ambacho kinaweza kuwa wazi iwapo Wandayi atapata kibali kutoka kwa Bunge la Kitaifa kujiunga na Baraza la Mawaziri la Ruto.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved