logo

NOW ON AIR

Listen in Live

ODM haijajiunga na serikali ya Ruto - Sifuna

Sifuna,alitaja uamuzi wa wanne hao kujiunga na baraza la mawaziri la Ruto kuwa wa kibinafsi.

image
na Davis Ojiambo

Habari25 July 2024 - 06:27

Muhtasari


  • •Sifuna alisema hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na chombo chochote cha chama kilichoidhinisha kujiunga kwa serikali ya Rais Ruto.
  • •Sifuna alishutumu vyombo vya habari kwa kupotosha msimamo wa chama cha ODM kuhusu suala hilo.

Katibu mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna ameshikilia kuwa chama chao hakijajiunga na serikali ya Rais William Ruto.

Kwenye mazungumzo na runinga ya Citizen,Sifuna alisema hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na chombo chochote cha chama kilichoidhinisha kujiunga kwa serikali ya rais Ruto.

“Kama katibu mkuu nakaa katika vyombo vyote vya chama na mimi ndiye msemaji wa vyombo vyote hivyo, Wakenya wanataka tu mtu awaambie ukweli na kumekuwa na minong’ono mingi kuhusu umuhimu wa kilichotokea jana," Sifuna alisema.

"Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna uamuzi wa chombo chochote cha ODM ambacho nitakaa kujiunga na serikali ya Ruto."

Aliendelea kusema kuwa kumekuwa na juhudi za kimakusudi za kukipaka chama cha ODM sura mbaya tangu kinara wa chama Raila Odinga alipohudhuria kutia saini mswada wa IEBC kuwa sheria katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Kenyatta (KICC).

Sifuna alishutumu vyombo vya habari kwa kupotosha msimamo wa chama hicho kuhusu suala hilo.

"Nadhani kumekuwa na juhudi za makusudi za kupotosha msimamo wa chama, haswa katika vyombo vya habari," aliongeza.

"Sijafurahishwa na jinsi vyombo vya habari vimechagua kuripoti mambo ambayo yametokea katika wiki chache zilizopita."

Alisema chama cha ODM huitisha tu mazungumzo ya kitaifa lakini hilo limegeuzwa kumaanisha mazungumzo kati ya ODM na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).

Matamshi yake yanakuja  baada ya rais Ruto kuwateua naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, mwenyekiti John Mbadi na kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi kujiunga na baraza lake la mawaziri.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved