Kiongozi wa chama cha Azimio Raila Odinga ametoa taarifa baada ya Rais William Ruto kuwateua viongozi wanne wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kwenye baraza la mawaziri.
Katika taarifa mnamo Julai 25, Raila alikubali uteuzi wa wanachama wanne wa chama chake kwenye baraza la mawaziri.
"Nimezingatia tangazo la Rais William Ruto jana kuhusu kuundwa upya kwa baraza la mawaziri kujumuisha wanachama wanne kutoka ODM," ilisema taarifa hiyo kwa sehemu.
Raila alishikilia kuwa uteuzi huo haukuwa sehemu ya makubaliano yoyote kati ya Ruto, chama chake au Azimio la Umoja.
"Kama ilivyobainishwa katika taarifa yetu ya Jumanne, Julai 23, 2024, si Chama cha ODM wala Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party ambayo imeingia katika makubaliano yoyote ya muungano na chama cha UDA cha Rais Ruto."
Raila alitaja kuwa chama kilitarajia kubuniwa kwa mashirikiano ya wazi kulingana na masuala mbalimbali.
"Ingawa tunawatakia kila la kheri walioteuliwa na kuamini kwamba watachangia vyema katika maendeleo ya taifa, tunaendelea kutetea ushirikiano wa kitaifa chini ya masharti yaliyoainishwa hapo awali," alisema.
Ruto aliwateua mwenyekiti wa ODM John Mbadi, kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi, Ali Hassan Joho, na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.
Zaidi ya hayo, Raila alidai kuachiliwa kwa watu wote walioko kizuizini na kukomesha kesi zote zinazohusiana na maandamano tangu mwaka jana. Raila pia anataka mashtaka ya polisi waliohusika katika kufyatua risasi kuwaua au kuwalemaza waandamanaji.