Wakaazi wa Ugenya Kaskazini, katika Kaunti ya Siaya wana sababu ya kutabasamu baada ya wanajeshi wa zamani wa KDF, chini ya mwavuli wa Veterans for Peace, wakichimba visima ili kukabiliana na uhaba wa maji katika eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Veterans For Peace Nelson Sechere ameeleza kuwa eneo hilo linakumbwa na maradhi yatokanayo na maji kutokana na maji yasiyo salama, na mpango huu utasaidia kutokomeza magonjwa hayo.
"Utafiti yakinifu uliofanyika katika Kaunti ya Siaya unaonyesha kuwa eneo hilo linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, na mpango huu utasaidia kukabiliana na hali hiyo," alisema Sechere.
Sechere pia alifichua kwamba maveterani hao wamejitolea kuchimba zaidi ya visima 300 kote nchini, huku kaunti za Mombasa, Makueni, Narok, na Kisii zikipewa kipaumbele.
Waziri (CEC) wa Maji wa kaunti ya Siaya, Prof. Jaqueline Oduol, alipongeza mpango huo, akisisitiza haja ya programu jumuishi ili kuhakikisha wakazi wanapata maji.
"Programu za maji na usafi wa mazingira ni kipaumbele cha juu katika Kaunti ya Siaya. Wakaazi wanateseka, huku wengi wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta bidhaa hii ya thamani," Oduol alisema.
CEC wa Afya (Kanali) Dkt. Martin Odhiambo K’onyango aliongeza kuwa kaunti itashirikiana na washikadau wote ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa wote.
Kisima kipya kilichochimbwa huzalisha ujazo wa lita 8,000 za maji kwa siku, zenye uwezo wa kuhudumia watu 2,000 kila siku.
MCA wa Ugenya Kaskazini pia alihudhuria hafla hiyo na kupendekeza kuwa miradi yote ya maji ijumuishe michakato ya usafishaji ili kufanya maji kuwa salama kwa matumizi ya binadamu, mifugo, na kilimo-hai.
Mwaka wa 2022, Kaunti ya Siaya ilikumbwa na uhaba mkubwa wa maji, na kuwalazimu wakaazi kutembea kilomita kadhaa kutafuta maji.
Tatizo linaendelea katika baadhi ya maeneo ya Siaya, huku wakazi bado wakitegemea madimbwi na mito kupata maji.