Mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimesema takriban watu tisa wamefariki kutokana na mkanyagano kwenye tamasha lililohudhuriwa na watu wengi kupita kiasi.
Tamasha hilo la mwanamuziki wa nyimbo za Injili Mike Galambay lilikuwa likifanyika katika uwanja wa Martyr katika mji mkuu, Kinshasa, Jumamosi.
Kulingana na vyombo vya habari nchini humo, watoto kadhaa wanaripotiwa kuwa miongoni mwa watu waliofariki, huku watu wengine wakilazwa katika wodi za wagonjwa mahututi baada ya ajali hiyo.
Gavana wa Kinshasa, Daniel Bumba, ametoa taarifa kulaumu kitendo cha kuwepo kwa watu wengi kupita kiasi.
Waandaaji wa tamasha hilo, Maajabu Gospel, wamesema maafisa wa usalama walijaribu kuwatuliza watu waliokuwa wanaleta vurugu, kitendo ambacho kimesabisha watu kupoteza maisha yao.
Waandaji wameongezea kusema kuwa uwanja wa Martyr, ambao unachukua watu 80,000, ulikuwa na watu 30,000 katika tanasha hilo lililofanyika siku ya Jumamosi.
Ajali sawia na hili lilitokea mwaka 2022 kwenye tamasha la mwanamuziki Fally Ipupa ambapo watu 11 walipoteza maisha.