logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Familia zilizohamishwa na mafuriko Tana River kupata makao mapya- Ruto

Baadhi ya wakazi walilazimika kutafuta hifadhi katika shule katika mji jirani wa Garissa.

image

Habari29 July 2024 - 14:02

Muhtasari


  • Kufikia Aprili 18, Umoja wa Mataifa uliripoti vifo vya angalau 32, watu 15 kujeruhiwa na wawili walipotea nchini kote.
Rais William Ruto

Rais William Ruto ameahidi kuwajengea nyumba mpya waliofurushwa na mafuriko ya mwaka huu katika kaunti ya Tana River.

Ruto alisema kuwa serikali imetenga Sh300 milioni kuwezesha ujenzi wa nyumba hizo mpya.

"Wale ambao nyumba zao ziliharibiwa na mafuriko watapata nyumba mpya. Serikali imetenga Sh milioni 300 kwa mradi huu," Ruto alisema.

Ruto alikuwa akizungumza huko Ngao, Kaunti ya Tana River, Jumatatu ambapo alizindua miradi tofauti.

Rais pia alisema kuwa serikali imejitolea kuboresha kilimo katika Tana River kwa kuboresha kiwango cha uzalishaji wa mahindi, mpunga na mboga.

“Tunataka Tana River izidi kukua katika sekta ya kilimo kupitia kulima mahindi, mpunga na mboga kwa wingi,” akasema Rais Ruto.

Maelfu ya wakaazi wa Mororo, Bakuyu na Ziwani kaunti ya Tana River walilazimika kuyahama makazi yao baada ya River Tana kuvunja kingo zake mwezi Aprili.

Baadhi ya wakazi walilazimika kutafuta hifadhi katika shule katika mji jirani wa Garissa.

Kulingana na Pius Mutuku, mtaalamu wa magonjwa katika Wizara ya Afya, visa 44 vya kipindupindu viliripotiwa Mei 2024 katika kaunti hiyo.

Kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zaidi ya watu 69,000 walikuwa wameathiriwa na mafuriko katika Kaunti ya Tana River kufikia Mei, 10,2024.

Kufikia Aprili 18, Umoja wa Mataifa uliripoti vifo vya angalau 32, watu 15 kujeruhiwa na wawili walipotea nchini kote.

Wakulima katika Tana River walipoteza mamia ya ekari za mazao ya shambani mwaka jana mafuriko yalipotokea wakati walikuwa karibu kuvuna mazao hayo.

Wafugaji nao hawakuachwa, hata hivyo, kwa vile vijiji vyao vilisongwa na hivyo kulazimika kuhama kwa wingi na chochote walichoweza kubeba, wakisema wanahama na hawatarudi tena.

Mbunge wa Garsen Ali Wario, ambaye alishuhudia vuguvugu hilo aliahidi kuwasaidia kujenga upya nyumba zao na kuishi katika maeneo yao mapya kabisa.

 

 

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved