Takriban watu 45 wameuawa na wengine kadhaa wanahofiwa kukwama baada ya mvua kubwa kusababisha maporomoko makubwa ya ardhi katika jimbo la Kerala kusini mwa India.
Maporomoko ya ardhi yamekumba maeneo ya vilima katika wilaya ya Wayanad alfajiri ya Jumanne.
Shughuli za uokoaji zinaendelea, lakini zinatatizwa na mvua kubwa na kuporomoka kwa daraja muhimu.
"Tutaweza kutathmini ukubwa wa uharibifu baada ya saa chache," waziri wa serikali AK Saseendran aliambia kituo cha BBC Hindi.
Bw Saseendran alisema hospitali za eneo hilo zilikuwa zikiwahudumia takriban watu 66 waliojeruhiwa, akiongeza kuwa wafanyikazi wa hospitali hiyo ni miongoni mwa waliotoweka kwenye maporomoko hayo.
Wayanad, wilaya yenye vilima ambayo ni sehemu ya safu ya milima ya Western Ghats, inakabiliwa na maporomoko ya ardhi wakati wa msimu wa monsuni.
Timu za serikali na za kitaifa zinaendesha shughuli za uokoaji. Wenyeji kadhaa pia wamekuwa wakisaidia.