Waandamanaji wa Israel wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia walivamia kambi ya jeshi wakionyesha uungaji mkono kwa wanajeshi wanaotuhumiwa kumdhulumu vikali mfungwa wa Kipalestina.
Umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya jengo la Sde Teiman baada ya polisi wa Israel kuingia humo kuwazuilia askari wa akiba, ambao sasa wapo chini ya uchunguzi rasmi.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa taarifa akilaani vikali tukio hilo na kutoa wito wa "kutulizwa kwa hasira mara moja".
Waandamanaji pia walivunja kambi ya pili ya kijeshi, ambapo askari wa akiba walipelekwa kuhojiwa, lakini msemaji wa polisi alisema maafisa waliweza kutuliza hali
Kambi ya Sde Teiman, iliyopo karibu na Beersheba kusini mwa Israel, kwa miezi kadhaa kumekuwa na ripoti za unyanyasaji mkubwa dhidi ya wafungwa wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya ndani, takriban wanajeshi tisa wa Israel katika kambi hiyo wanatuhumiwa kumtusi mfungwa huyo wa Kipalestina, anayeshukiwa kuwa mpiganaji wa Hamas ambaye alitekwa Gaza.
Inasemekana amelazwa hospitalini baada ya kile ripoti za vyombo vya habari vya Israel kueleza kuwa ni unyanyasaji mkubwa wa kingono na majeraha kwenye sehemu yake ya haja kubwa na kusababisha kushindwa kutembea.
Jeshi la Israel lilisema wakili wake mkuu aliamuru uchunguzi "kufuatia unyanyasaji mkubwa wa mfungwa".
Tume ya Masuala ya Wafungwa ya Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi (PA) ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kwa haraka kwa kufanya uchunguzi ulioamriwa na Umoja wa Mataifa.