Kindiki Kithure ambaye amependekezwa kuwa waziri wa usalama amesema idara ya polisi inafaa kuajibikia dhulma zozote wakati wa maandamano ya Gen-Z.
Wakati akipigwa msasa na kamati ya bunge ya uteuzi Kindiki ambaye alikuwa waziri wa usalama wakati wa maandamano ya Gen-Z alisema idara ya polisi ni huru na haifai kufuata maagizo ya mtu yeyote ila kutoka kwa Inspekta Jenerali.
Akiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Uteuzi wakati wa kikao cha uhakiki, Kindiki alieleza kuwa huduma ya polisi ni ofisi huru inayofanya kazi chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali.
Alisema kuwa kazi yake ni kutoa miongozo ya sera kwa vyombo vya usalama wa taifa kama ilivyoainishwa katika Katiba.
Kindiki alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed aliyehoji ni kwa nini Waziri alinyamaza wakati wa maandamano ya Gen Z huku waandamanaji wakitekwa nyara na kuuawa.
"Polisi wako chini ya amri huru. Kuna watu wawili tu ambao wanaweza kutoa maagizo ya IG: Waziri wa Mambo ya Ndani (kuhusu masuala ya sera) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuhusu uchunguzi wa uhalifu."
Alikiri vifo na kukamatwa kwa watu wakati wa maandamano lakini akapongeza polisi kwa juhudi zao wakati wa maandamano. Alibainisha kuwa ni Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) kuchunguza na kuwashtaki maafisa waovu waliotumia nguvu kupita kiasi.
Alisikita kwamba katika maandamano ya hivi majuzi, kulishuhudia vifo vya Wakenya 42, raia 486 na polisi 285 kujeruhiwa. Jumla ya watu 1,387, magari 54 ya polisi na mengine 110 ya kibinafsi yaliharibiwa.
Kindiki alisema kila afisa wa polisi anafaa kuajibikia matendo yake na wala si kutupia lawama huduma nzima ya polisi.
"Suala la matumizi ya silaha kwa askari ni la mtu binafsi. Afisa yeyote ana jukumu la mtu binafsi jinsi ya kutumia silaha zake. Uwajibikaji wa Inspekta Jenerali ni juu ya utaratibu wa oparesheni lakini matumizi ya nguvu ni jukumu la mtu binafsi," alisema.