Mteule wa Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Aden Duale amefichua kuwa thamani yake kwa sasa ni Sh980 milioni.
Duale akizungumza alipofika kupigwa msasa na Kamati ya Bunge ya Uteuzi, Duale alisema utajiri wake ni wa mali pamoja na uwekezaji.
"Nina vipande vya ardhi Garissa na Nairobi, Nyumba yangu Nairobi, nyumba yangu huko Garissa, shamba langu la Ng'ombe huko Garissa, mali yangu ya kukodisha huko Nairobi na Garissa, hisa zangu katika biashara zinazomilikiwa na familia, Ngamia na ng'ombe wangu, na magari,” Duale alisema.
"Mwisho, nilipata mapato mazuri kutokana na mauzo ya kitabu cha Wasifu wangu ambacho ni mojawapo ya vitabu vinavyouzwa zaidi leo,"
Wakati akipigwa msasa mnamo Oktoba 2022, Duale alisema thamani yake wakati huo ilikuwa Sh851 milioni.
"Mwenyekiti, nina thamani ya Sh851 milioni ikiwa ni pamoja na mali ninayomiliki. Ikiwa ni pamoja na mbuzi, kondoo na ngamia ambao ninamiliki nililazimika kwenda kuthamini ngamia wangu 231 mahali fulani katika kaunti ya Kitui," alisema kisha.
Pia alisema mapato yake wakati huo yalikuwa takriban Sh10 milioni, kila mwaka.
Duale alieleza kuwa ukuaji wa mali yake ulitokana na kuthaminiwa kwa ardhi yake na uwekezaji na mali isiyohamishika.
Aliongeza kuwa mifugo yake pia iliongezeka kwa sababu ya msimu mzuri.
"Tulikuwa na mvua nzuri sana mifugo yangu iliongezeka kwa idadi."
Duale alihamishwa hadi kwenye hati ya Mazingira na Rais William Ruto baada ya kuteuliwa kurejea kwenye baraza la waziri.