Naibu
Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua ameibua madai kuwa kulikuwa na majaribio
mawili ya kumuua ambayo hayakufaulu kabla ya mpango wa kumuondoa madarakani
kutekelezwa.
Wakati
akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Karen mnamo
Jumapili, Oktoba 20, Gachagua alidai kuwa baadhi ya mashirika ya usalama
yalijaribu kumuua mara mbili lakini ikashindikana.
Alibainisha
kuwa jaribio la kwanza lilikuwa Kisumu mwishoni mwa Agosti ambapo aliwekewa
sumu kwenye chakula chake kabla ya timu yake kugundua.
"Mnamo
Agosti 30, huko Kisumu, maafisa wa usalama waliofichwa waliingia chumbani
kwangu na kukivamia na mmoja wao akajaribu kutia sumu kwenye chakula changu,
lakini tuligundua na tukaweza kutoroka mpango huo. Ilipangwa niuawe kwa sumu ya
chakula, " Gachagua alisema.
Mwanasiasa
huyo alidai kuwa jaribio la pili la mauaji lilijiri siku chache baadaye katika
kaunti ya Nyeri na lilitekelezwa na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi.
“Mnamo Septemba 3, timu nyingine kutoka Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi ilifika Nyeri na kujaribu kutia sumu kwenye chakula ambacho kilikusudiwa mimi na baraza la wazee wa Kikuyu,” alisema.
Aliongeza,
"Niliripoti suala hili kwa NIS na kuwataka maafisa waliopewa kazi katika
afisi yangu kuondoka kwa sababu nilihisi siko salama. Baada ya majaribio hayo
mawili ya mauaji kufeli, ndipo hoja hii ya kunitimua ilipoasisiwa.”
Akiwahutubia
wanahabari, Gachagua pia alifichua kuwa maafisa wake wa usalama waliondolewa
mara moja siku ambayo alipotimuliwa na bunge la seneti la Kenya.