Naibu rais aliyetimuliwa Geoffrey
Rigathi Gachagua amezungumza kwa mara ya kwanza hadharani tangu maseneta
wamuondoe ofisini siku ya Alhamisi.
Huku akiwahutubia wanahabari nje
ya Hospitali ya Karen mnamo Jumapili, Oktoba 20, 2024, Gachagua alithibitisha
kuwa kweli aliugua baada ya seneti kuchukua mapumziko ya mchana siku ya Alhamisi.
Gachagua alisema kuwa baada ya
seneti kwenda mapumziko, alikwenda kula chakula cha mchana pamoja na mawakili
wake na viongozi wengine kabla ya kuamua kupita ofisini kwake kuchukua karatasi
alizohitaji. Anasema kuwa alipokuwa akielekea ofisini kwake ndipo alianza
kusikia maumivu kifuani.
"Wakati nilikuwa naenda
ofisini ghafla nilipata maumivu makali sana kwenye kifua. Nilikaa chini na
maumivu yakaendelea, yalikuwa makali sana na makali sana,” Rigathi Gachagua
alisema.
Aliendelea, “Nilimpigia simu
daktari wangu Dkt. Gikonyo wa hospitali hii ambaye amekuwa daktari wangu kwa
miaka 20 iliyopita na nilimweleza kwa ufupi jinsi nilivyokuwa nikihisi.
Aliniuliza kuhusu ukali wa maumivu nikamwambia ni makali sana. Tukiwa tunaongea
nilianza kukosa pumzi. Dkt. Gikonyo
aliniagiza kuacha kila kitu nilichokuwa nikifanya na kufika hapa kwa Karen
haraka iwezekanavyo. Aliniambia nilichokieleza si kitu kizuri, na ni lazima
nije hapa.”
Naibu rais huyo aliyetimuliwa
anasema kwamba aliheshimu maagizo ya daktari mara moja na akakimbizwa katika
Hospitali ya Karen na timu yake.
Anaongeza kuwa madaktari katika
Hospitali ya Karen walifanikiwa kumtuliza lakini akabainisha kuwa walionya
kwamba ingekuwa mbaya zaidi ikiwa hangefika hospitalini kwa wakati.
"Baada ya kupata utulivu,
daktari aliniambia kuwa kama ningechelewa kwa dakika 20, tungezungumza hadithi
nyingine leo," alisema.
Naibu
rais aliyetimuliwa alisema kuwa ingawa hajapona kabisa, sasa anahisi vizuri na
yuko nje ya hatari.
"Maumivu makali yamepita. Kilichopo kinaweza kudhibitiwa kwa mwanaume. Mwanaume lazima awe na uwezo wa kustahimili baadhi ya mambo haya madogo. Katika tathmini yake (daktari), niko nje ya hatari. Lakini nilipokuja ilikuwa kali sana,” alisema.