logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Gachagua aomboleza kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Tharaka Nithi

Marehemu Nkatha alifariki wiki jana alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Misheni ya St Theresa's Kiirua.

image
na SAMUEL MAINAjournalist

Habari21 October 2024 - 08:41

Muhtasari


  • Gachagua mnamo Jumapili jioni aliomboleza kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Tharaka Nithi, marehemu Beatrice Nkatha Nyaga.
  •  Naibu rais huyo aliyetimuliwa alizungumzia uhusiano mzuri aliokuwa nao na Bi Nkatha walipohudumu pamoja katika Bunge la 12.

Naibu Rais aliyetimuliwa Geoffrey Rigathi Gachagua mnamo Jumapili jioni aliomboleza kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Tharaka Nithi, marehemu Beatrice Nkatha Nyaga.

 Marehemu Nkatha, ambaye alihudumu kwa mihula miwili kati ya 2013 na 2022, alifariki wiki jana alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya St Theresa's Kiirua Kaunti ya Meru. Alikuwa akipambana na ugonjwa kwa muda mrefu.

 Huku akimuomboleza marehemu mwanasiasa huyo, Gachagua alimtaja kama kiongozi aliyezingatia watu na alitekeleza majukumu yake vyema.

 Ilikuwa ni huzuni kubwa nilipopata habari kuhusu kufariki kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Tharaka Nithi Mhe. Beatrice Nkatha Nyaga. Mhe Nkatha alikuwa mtumishi mwenye urafiki, kiongozi aliyezingatia watu ambaye alijishughulisha na lolote ili kutoa kilicho bora zaidi katika kutekeleza majukumu yake,” Gachagua aliomboleza.

 Naibu rais huyo aliyetimuliwa aliendelea kuzungumzia uhusiano mzuri aliokuwa nao na Bi Nkatha walipohudumu pamoja katika Bunge la 12.

  “Wakati tulipohudumu pamoja katika Bunge la 12, nilimfahamu Mhe. Nkatha kama kiongozi mwadilifu na kama rafiki mama na wa dhati,” alisema.

 Aliongeza, “Tumempoteza kiongozi mpenda mabadiliko.  Mola awape faraja familia yake, ndugu jamaa na marafiki.  Pumzika kwa Amani Mhe. Nkatha.”

 Marehemu Nkatha anayetoka eneo la Chuka-Igambang'ombe katika kaunti ya Tharaka Nithi anaripotiwa kuugua kwa muda kabla ya kuaga dunia wiki jana.

 Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, Mbunge wa Tharaka Gitonga Murugara na Spika wa Bunge John Mbabu ni miongoni mwa viongozi waliomuomboleza marehemu Mwakilishi wa Kike huyo wa zamani kufuatia habari za kifo chake.

 Marehemu mwanasiasa huyo alisifiwa kama kiongozi aliyeepuka mabishano na kuathiri vyema jamii alizohudumu.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved