WAZIRI wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen ametoa onyo kali kwa vijana wanaotumia mitandao kwa njia mbaya ya kuweka picha za viongozi kwenye majeneza.
Akizungumza katika
kaunti ya Uasin Gishu alikoandamana na rais Ruto katika ziara ya kimaendeleo ya
siku 3 iliyoanza Alhamisi kwenye bonde la Ufa, waziri huyo alisema kwamba yeye
kama waziri wa usalama wa ndani ataangalia upya suala hilo na kuwachukulia
hatua wahusika.
Seneta huyo wa zamani wa
Elgeyo Marakwet alisisitiza kwamba kuna umuhimu wa viongozi na haswa kiongozi
wa taifa kuheshimiwa, akisema kwamba kuweka picha yake kwenye jeneza ni
kiashiria cha kutishia maisha yake.
Murkomen aliwalaumu
wazazi na baadhi ya viongozi wa kidini wanaowakingia vifua vijana wa kueneza
picha hizo za AI kwamba wamefeli kwani tabia hiyo si ya kufurahikiwa bali ya
kukemewa.
“Ukiona wale
wanatengeneza picha kama wameweka mtu kwa jeneza, na wanaweka kwenye jeneza
kiongozi wa taifa, mimi nataka nilize, nan ataka kuuliza swali hili kwa kila
mzazi humu nchini, na haswa viongozi wa kanisa wanaotetea hii tabia mbaya, na
wanasiasa wote ikiwemo wale tusiokubaliana kisiasa, ikiwa kesho mwanao anaenda
shule na kukutana na mwenzake ambaye wanashiriki darasa moja amemchora kwenye
jeneza, bado utatetea hiyo tabia?” Murkomen aliuliza.
“Kwa sababu wakati picha
kama hiyo inapowekwa, inatuma ujumbe wa kutishia kwamba nitakuuwa. Natuko hapa
tunapigia makofi tabia ambazo zimeendelezwa kwa muda mrefu.”
“Ningependa
kukuhakikishia mheshimiwa rais, mimi mwenyewe na timu yetu kwenye wizara ya
usalama wa ndani, tunaenda kuliangalia upya suala hili na kuhakikisha
tunawachukulia hatua kwa sababu kama hatuwezi kufanya hivyo, hatutakuwa na nchi
yenye muongozo mzuri,” Murkomen alisema.