Baba na mama wa kambo watiwa mbaroni kwa kumtesa mtoto wa miaka 6 hadi kufa

Muhtasari

•Robinson Musyoki na mkewe Rose Muteti walikamatwa nyumbani kwao Emali, Makueni Jumapili baada ya kubainika walimtesa Beverly Mumo Musyoki hadi kifo.

•Kesi ya mauaji ya Mumo ilikuwa imetupiliwa mbali kwa madai kuwa aliangamizwa na mapepo ila wapelelezi wa mauaji wakairejelea tena na kufanikiwa kuitatua.

•Wapelelezi wamebaini kuwa ndugu ya marehemu wa miaka 11 ambaye alishuhudia yaliyotukia alikuwa ametishiwa maisha endapo angesema ukweli.

Robinson Musyoki na Rose Muteti
Robinson Musyoki na Rose Muteti
Image: TWITTER// DCI

Wanandoa wawili wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji katika mahakama kuu ya Machakos baada ya uchunguzi kubaini walihusika katika mauaji ya mtoto wa miaka 6 mnamo Agosti 24, 2020.

Robinson Musyoki na mkewe Rose Muteti walikamatwa nyumbani kwao Emali, Makueni Jumapili baada ya kubainika walimtesa Beverly Mumo Musyoki hadi kufa.

Hapo awali kesi ya mauaji ya Mumo ilikuwa imetupiliwa mbali kwa madai kuwa aliangamizwa na mapepo ila wapelelezi wa mauaji wakairejelea tena na kufanikiwa kuitatua.

Kulingana na DCI, Bi Naomi Kiamba ambaye ni mama mzazi wa Mumo alifahamu kuhusu kifo chake mnamo Oktoba 24, 2020 baada ya Musyoki kumpigia simu na kumuarifu kuwa bintiye alifariki kutokana na ugonjwa.

Naomi alifahamishwa kuwa mwili wa bintiye ulikuwa umehifadhiwa katika mochari ya Montezuma na akaelekea pale ili kudhibitisha. Alipofika pale aliona mwili wa Mumo ukiwa umejaa michimbuko ya mateso.

Kipindi Mumo alikutana na mauti yake alikuwa anaishi na babake baada ya mahakama ya watoto kumwagiza akae naye kwa takriban mwaka mmoja kabla ya kurejeshwa kwa mamake.

Ndoa yao ilivunjika baada ya tabia za Musyoki kubadilika ghafla na kumpelekea Naomi kukumbwa na msongo wa mawazo. Baada ya kutengana kwao Musyoki alijitosa kwenye mahusiano mengine na kuhamia kwingine.

Baada ya mahakama kumwelekeza Musyoki kuishi na bintiye kwa kipindi cha mwaka mmoja Naomi hakuwahi kumwona tena hadi alipopokea habari za kifo chake.

Wapelelezi wamebaini kuwa ndugu ya marehemu wa miaka 11 ambaye alishuhudia yaliyotukia alikuwa ametishiwa maisha endapo angesema ukweli.

Kwa sasa washukiwa wanazuiliwa na wanatarajiwa kujibu mashtaka ya mauaji.