SIASA ZA JUJA

Gavana Nyoro akanusha madai ya kusababisha vurumai Mang'u

Amesema kuwa yeye sio mtu wa vurugu na wapinzani ndio waliojaribu kumnyamazisha alipojaribu kutoa malalamishi

Muhtasari

•Gavana amesema kuwa atakubali matokeo

•Adai kuwa yeye sio mtu wa vurugu

James Nyoro
James Nyoro

Gavana wa kaunti ya Kiambu James Nyoro amekanusha madai ya tume ya IEBC kuwa aliongoza kikundi cha wahuni kilichosababisha vurumai katika kituo cha kuhesabu kura cha Mangu.

Gavana huyo ambaye aliridhi kiti hicho baada ya aliyekuwa gavana mchaguliwa, Ferdinard Waititu kutimuliwa ameeleza kuwa alikuwa anatoa malalamishi kuwa kura toka vituo mbili ambazo mgombeaji na chama cha Jubilee alikuwa na ushawishi mkubwa  hazikuwa zimehesabiwa.

Nyoro ameeleza kuwa wapinzani wa mgombeaji wa Jubilee, Susan Njeri walianza kuwanyamazisha alipojaribu kutoa malalamishi yake.

“Napinga vikali madai kuwa mimi ni mtu wa vurugu. Sijawai kuwa mwenye vurugu hata kwenye kipindi cha kampeni zangu. Hatukusika kamwe kwenye vurumai ile” Nyoro alisema.

Usiku wa kuamkia Jumatano, IEBC ilkuwa imesimamisha shughuli ya kuhesabu kura kwa madai kuwa Nyoro alikuwa amesababisha vurugu kura zilipokuwa zinahesabiwa. Kwenye video zinazosambazwa mtandaoni, gavana Nyoro anaonekana kupinga shughuli za uhesabu kura huku akisema hawatakuli matokeo kwani walishuku kuna wizi uliotendeka.

Akiongezea, gavana Nyoro ametangaza kuwa angekubali matokeo huku akisema sio shughuli yake kutoa malalamishi yoyote kuhusu shughuli hiyo ila ni kazi ya chama cha Jubilee.

Upande wake mgombeeaji na tikiti ya PEP, George Koimburi, pia ulikuwa umemsuta vikali gavana huyo kwa madai ya uchochezi dhidi yao. Wakiongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, walilaani kitendo cha gavana huyo huku wakitishia kuanzisha mpango wa kumng’atua mamlakani.