Afueni! Rais Kenyatta aondoa kafyu ya kitaifa

Muhtasari

• rais amesema kwamba hatua hiyo imefikiwa kufuatia maendeleo mazuri katika kuthibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

•Rais vilevile ameelekeza idadi ya waumini ambao wanaweza kujumuika pamoja  kanisani iongezewe kutoka thuluthi moja hadi thuluthi mbili.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiongoza sherehe za Mashujaa, 20/10/2021 Picha: PSCU
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiongoza sherehe za Mashujaa, 20/10/2021 Picha: PSCU

Wakenya wameweza kupata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoa kafyu ya usiku ya kitaifa ambayo imekuwepo tangu mapema mwaka uliopita.

Rais ametoa amri kwamba kafyu ambayo iliwekwa mwezi Machi mwaka uliopita kufuatia mkurupuko wa maradhi ya COVID 19 iondolewe mara moja kuanzia usiku wa Jumatano.

Alipokuwa anatoa hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Mashujaa ambayo yalifanyika katika uwanja wa Wang'uru kaunti ya Kirinyaga, rais amesema kwamba hatua hiyo imefikiwa kufuatia maendeleo mazuri katika kuthibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

"Kulingana na madaraka ambayo nimepatiwa kama rais, naamuru na kuelekeza kwamba kafyu ya kitaifa ya kutoka usiku hadi asubuhi ambayo imekuwepo tangu tarehe 27 Machi 2020 iondolewe mara moja" Rais aliamuru.

Kwa kipindi cha zaidi ya miezi 18 Wakenya wamelazimika kuwa ndani ya nyumba kabla ya saa nne usiku na kuruhusiwa kutoka baada tu ya saa kumi asubuhi kutimia kufuatia amri ya kukaa ndani iliyokuwa imewekwa.

Kando na kafyu ya kitaifa, rais vilevile ameelekeza idadi ya waumini ambao wanaweza kujumuika pamoja  kanisani iongezewe kutoka thuluthi moja hadi thuluthi mbili.

Hata hivyo, waumini wameagizwa kuzingatia mikakati iliyowekwa kuthibiti maambukizi kama vile uvaliaji wa barakoa na kunawa mikono kila mara.