Rais wa FKF Nick Mwendwa akamatwa kwa madai ya kuvuja pesa za FKF

Muhtasari
  • Rais wa FKF Nick Mwendwa akamatwa kwa madai ya ufisadi
  • Mwendwa alichukuliwa na magari mawili ya polisi na kutakiwa kumwita wakili wake
  • Mnamo Alhamisi, Mwendwa alipuuzilia mbali kamati ya muda iliyoteuliwa na CS Amina kuendesha soka nchini
Rais wa FKF Nick Mwendwa

Rais wa Shirikisho la kandanda nchini Nick Mwendwa amekamatwa na kupelekwa katika makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika Barabara ya Kiambu kuhojiwa.

Kulingana na ripoti, Mwendwa alikamatwa muda mfupi baada ya kutoka katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi ambako alikuwa akifuatilia kesi ya kupinga kuvunjwa kwa FKF na serikali.

“Yeye (Nick Mwendwa) yuko Mazingira House ambapo wapelelezi wetu wanamhoji. Tutatoa taarifa baadaye,” alisema msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Bruno Shioso.

Maafisa walisema tukio hilo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu madai ya ufisadi katika sekta hiyo.

Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia suala hilo wanasema pia watazungumza na maafisa wengine wa FKF.

Mwendwa alichukuliwa na magari mawili ya polisi na kutakiwa kumwita wakili wake.

Mnamo Alhamisi, Mwendwa alipuuzilia mbali kamati ya muda iliyoteuliwa na CS Amina kuendesha soka nchini.

Mkali huyo wa FKF aliapa kupambana na majaribio yoyote ya kuuondoa uongozi wake wa miaka mitano ofisini.