FKF:Nick Mwendwa aachiliwa kwa dhamana, azuiliwa kuingia kwenye ofisi za FKF

Muhtasari
  • Bosi huyo wa FKF aliyesimamishwa kazi pia alizuiwa kuingia katika ofisi ya FKF au kuhudhuria shughuli zozote za soka
Image: MAKTABA

Rais wa FKF Nick Mwendwa ameachiliwa kwa bondi ya Ksh7 milioni akiwa na wadhamini wawili au dhamana ya pesa taslimu ya Ksh4 milioni na watu wawili wa mawasiliano baada ya uamuzi wa mahakama siku ya Jumatatu, Novemba 15.

Bosi huyo wa FKF aliyesimamishwa kazi pia alizuiwa kuingia katika ofisi ya FKF au kuhudhuria shughuli zozote za soka, ukiwemo mchezo wa leo dhidi ya Rwanda, hadi mahakama itakapotoa uamuzi Jumatano, Novemba 17.

Wakati wa kesi katika Mahakama ya Milimani, upande wa mashtaka uliomba amri ya kumweka kizuizini Mwendwa kwa siku 14 ili kuwezesha maafisa kukamilisha uchunguzi kuhusu madai ya matumizi mabaya ya fedha.

Mwendwa hata hivyo, hakujibu mashtaka ya ulaghai baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kutaka kumweka kizuizini- akisema kuwa Mwendwa anaweza kuingilia uchunguzi unaoendelea.

"Mwendwa ana uwezekano mkubwa wa kuharibu au kuficha ushahidi unaofaa au kuingilia mashahidi na ukusanyaji wa ushahidi hivyo kuathiri uchunguzi iwapo ataachiliwa kwa sasa," timu ya waendesha mashtaka ilisema.

Timu yake ya wanasheria ilijumuisha aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK). Eric Mutua na Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior.

Mwendwa alikamatwa Ijumaa, Novemba 12, na kuhojiwa kwa saa nyingi na Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI).