Manchester United yamtimua kazini kocha Ole Gunnar Solkjaer kufuatia msururu wa matokeo hafifu

Muhtasari

•United imetangaza hatua ya kumtimua Solskjaer kazini kupitia  taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya klabu alasiri ya Jumapili.

•Kiungo wa kati wa zamani wa mashetani wekundu Michael Carrick  atashikilia nafasi iliyoachwa wazi na Solskjaer hadi mwisho wa msimu wa EPL 2021/22.

Ole Gunnar Solskjaer
Ole Gunnar Solskjaer
Image: BBC

Klabu ya Manchester United imefuta kazi kocha Ole Gunnar Solksjaer masaa machache tu baada ya kupoteza mechi  yake ya tano msimu huu.

United imetangaza hatua ya kumtimua Solskjaer kazini kupitia  taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya klabu alasiri ya Jumapili.

Klabu hiyo imemshukuru Solskjaer kwa huduma ambao ametoa katika kipindi cha miaka mitatu ambacho amehudumu kama meneja. 

"Manchester United inatangaza kwamba Ole Gunnar Solskjaer ameacha kazi yake kama meneja. Ole daima atakuwa gwiji wa Manchester United na ni kwa masikitiko kuona kwamba tumefikia uamuzi huu mgumu. Ingawa wiki chache zilizopita zimekuwa za kukatisha tamaa, hazipaswi kuficha kazi zote alizofanya katika kipindi cha miaka mitatu ili kujenga upya misingi ya mafanikio ya muda mrefu" United imetangaza.

Kiungo wa kati wa zamani wa mashetani wekundu Michael Carrick  atashikilia nafasi iliyoachwa wazi na Solskjaer hadi mwisho wa msimu wa EPL 2021/22.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mashetani wekundu kupoteza 1-4 ugenini dhidi ya Watford. 

Mechi hiyo iliyochezwa  Jumamosi jioni ilikuwa ya tano Manchester kupoteza msimu huu na iliongeza shinikizo kwa Solksjaer.

Mashabiki wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kushinikiza bodi ya United kumtimua Solksjaer kufuatia matokeo duni ambayo klabu hiyo imekuwa ikiandikisha hivi karibuni.

Solksjaer alijiunga na United mwezi Desemba mwaka wa 2018 akiridhi kiti hicho kutoka kwa aliyekuwa kocha mkuu Jose Mourinho ambaye alitimuliwa baada ya kutofautiana na bodi pamoja na wachezaji.