Mamlaka ya mawasiliano yaahirisha usajili wa sim card hadi Oktoba 15

Muhtasari

• Mamlaka wa mawasiliano nchini CA, imesongesha mbele mpango wake wa kukatisha huduma kwa wale ambao walikuwa hawajasajili  hadi Oktoba 15.

• Awali mamlaka hiyo ilikuwa imepanga kukatisha huduma za wateja ambao walikuwa hawajasajili kadio zao ifikiapo tarehe 14 mwezi Aprili.

 

Ezra Chiloba
Ezra Chiloba
Image: Twitter

Mamlaka ya mawasiliano nchini, CA imesongesha mbele kwa miezi sita  mpango wao wa kukatisha huduma kwa wateja ambao walikuwa hawajasajili kadi zao hadi tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka huu.

CA ilichukua hatua hiyo baada ya asilimia kubwa ya wakenya kufeli kusajili kadi zao ifikiapo tarehe 15 mwezi Aprili.

Wakenya sasa wana miezi sita kuhakikisha kwamba kadi zao zinasajiliwa.

Aidha, mamlaka hiyo ilitoa onyo kwamba wateja ambao kadi zao zitakuwa hazijasajiliwa watatozwa faini.

Haya yanajiri baada ya mkurugenzi wa CA, Ezra Chiloba kusema kwamba mamlaka hiyo itafanya mazungumzo na watoa huduma wa mitandao kuhusu uwezekano wa kusongesha mbele mchakato wa kusajili kadi ili kutoa muda zaidi kwa wateja kuhalalisha maelezo yote ya usajili.

Upanuzi huo pia ulifuatia mashauriano ya kina kati ya CA na watoa huduma za mitandao ya simu . Chiloba na MNOs walifanya mkutano Alhamisi, Aprili 14 ili kutathmini kiwango cha ufanisi wa zoezi hilo.

" Ni jukumu la watoaji huduma kushauri iwapo kadi za wale ambao hawajajisajili zitazimwa au tutatoa muda zaidi ili wakamilishe shughuli hiyo," Chiloba alisema.

 CA ilishikilia kuwa zoezi hilo la usajili limeainishwa katika katiba inayowaagiza watoaji huduma za mtandao wa simu kutekeleza zoezi hilo. Siku ya Ijumaa, Safaricom ilianza rasmi shughuli ya usajili wa kadi za simu.

Hii ni baada ya Wakenya kulalamika  kwenye mitandao ya kijamii, wakiomba kampuni hiyo kufuata nyayo za Telkom ambao walikuwa wameanzisha usajili wa Sim Card mtandaoni.