(VIDEO) IG Mutyambai - Polisi 2K hawafai kuhudumu, wana matatizo ya afya ya kiakili

Muhtasari

• Inspekta jenerali wa polisi Hillary Mutyambai alisema polisi 2000 wamepatikana na matatizo ya kuwafanya wasiwe sawa kuhudumu.

• Alisema pia wengine 690 walikuwa wakidanganya kuwa wagonjwa, akawaiita malingerers.

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai
Image: George Owiti

Jumanne, Inspekta jenerali wa polisi Hillary Mutyambai ametoa taarifa ya kushtusha kuhusu polisi.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa kidini na maaskofu wa Kianglikana jijini Nairobi, Mutyambai alisema kwamba baada ya tume ya huduma kwa polisi kuanzisha bodi ya kimatibabu kwa polisi na kuwapima maafisa wote wa polisi, afisa wa polisi 2000 walipatikana na matatizo mbali mbali yanayowafanya kutokuwa imara kuhudumu katika idara ya polisi.

“Tumeanzisha bodi ya kimatibabu ya polisi ambapo tuliwapima maafisa wote wa polisi na la kushangaza ni kwamba tulipata idadi kubwa sana ya maafisa elfu mbili ambao wako na hali zisizofaa kwa wao kuhudumu katika idara ya polisi,” Mutyambai alisema.

Mutyambai alisema kwamba sasa mchakato wa kuwaachisha kazi kisheria umeanza na kudokeza kwamba si rahisi kuachisha tu mtu kazi wakati tayari anahudumu kwa sababu sheria zipo na serikali ina mipangilio yake.

Inspekta jenerali huyo pia alisema kwamba walianza kufanya vipimo vya akili kwa maafisa wote kuanzia kiwango cha kuajiriwa kazi mpaka wakati wanaendelea kufanya kazi.

Alidokeza kwamba kunao wengine waliokuwa wakidanganya kwamba ni wagonjwa lakini kumbe ni kuigiza tu na ambao idadi yao ilikuwa kubwa.

“Tulipata pia maafisa wengine ambao walikuwa wanadai wako wagonjwa. Kati ya hiyo idadi tuliweza kuwapata maafisa 690 ambao walikuwa wanadai ni wagonjwa lakini kumbe ni kukwepa kazi, tunawaita malingerers. Kuna wengine wakisema ni wagonjwa ni wagonjwa kweli huku baadhi ni hawataki kufanya kazi na kusingizia ugonjwa. Ni kazi ngumu,” aliongeza Mutyambai.

Alisema kwamba afya ya kiakili kwa maafisa wa polisi ni jambo ambalo linazingatiwa kwa ukaribu kwa sababu tofauti na mwananchi wa kawaida, kifaa cha kazi kwa polisi ni bunduki na wasipochunguzwa kiakili vizuri risasi moja ikifyatuliwa huleta madhara makubwa.