Mohammed Ali - Kibaki alistaafu kimya kimya bila kumpigia debe mrithi wake, bei ya bidhaa ilikuwa nafuu

Muhtasari

• Mohammed Ali amemuomboleza Kibaki kama rais aliyestaafu kimya kimya bila kuonesha kumpigia debe mrithi wake.

Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, Mwai Kibaki
Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, Mwai Kibaki
Image: Twitter

Mbunge wa Nyali Mohammed Ali amemuomboleza hayati rais Mwai Kibaki kaam mtu ambaye hakupenda kusifiwa sana na umma kwani alikuwa anajua chochote alichokuwa akikifanya ni kwa ajili ya wananchi na si kutafuta sifa.

Ali ambaye anaegemea mrengo wa naibu rais William Ruto vile vile alitumia fursa hiyo kuukosoa uongozi wa sasa kwa lugha fiche ambapo alisema kwamba wakati wa Kibaki, uchumi ulikuwa umeimarika pakubwa kwani bei ya bidhaa kama vile petroli, mafuta ya kupika, unga na vingine zilikuwa chini na kufikiwa na wananchi kwa urahisi.

Mohammed Ali pia alitupia uongozi wa rais Kenyatta maneno aliposema kwamba rais Kibaki alistaafu kimya kimya bila kusema mrithi wake, bila shaka hili likiwa linamlenga kumchuna sikio rais Kenyatta ambaye anaondoka madarakani na ameonekana wazi akimpigia debe mgombea wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga.

Vile vile Ali aligusia kwamba Kibaki alifanya kazi kubwa pasi na kutaka sifa na kazi hizo, akitolea mfano barabara kuu ya Thika ambayo iliasisiwa na Kibaki, Ali alisema barabara hiyo haina mahali popote palipotundikwa jina lake kwamba ndiye kaijenga, bila shaka hili pia lilimlenga Raila Odinga ambaye miezi michache iliyopota barabara ya Mbagathi ilibadilishwa jina na kuitwa jina lake.