Rais Kenyatta - Kibaki aliheshimisha Kenya kimataifa kwa kustawisha uchumi

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta amemuomboleza hayati Mwai Kibaki kama mpiganaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya.

Rais wa 3 wa Kenya, Mwai Kibaki
Rais wa 3 wa Kenya, Mwai Kibaki
Image: Twitter

Rais Uhuru Kenyatta amemuomboleza mtangulizi wake kama mtu ambaye daima atakumbukwa kama mtu mwenye hekima aliyekuwa mchangiaji mzuri wa mijadala.

Kenyatta pia alisema kwamba Kibaki alichangia pakubwa katika ukombozi wa pili wa uhuru wa taifa la Kenya na kuwa mwezeshaji mkubwa aliyekuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa vyama vingi nchini na demokrasia Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta pia alimtaja hayati Mwai Kibaki kama kiongozi aliyepiga hatua kubwa ya kuunganisha muungano wa mataifa ya Afrika Mashariki hatua ambayo iliimarisha uchumi wa taifa hili.

“Kujitolea kwake na mapenzi yake ya dhati kwa kweli yaliiheshimisha Kenya katika ukanda wa Afrika Mashariki, bara la Afrika na dunia yote kwa ujumla,” Rais Kenyatta aliomboleza.

Rais Kenyatta alitangaza maombolezo ya kitaifa kwanzia Ijumaa hadi siku ya maziko yake na pia kutangaza bendera zote kupeperushwa nusu mlingoti.

Rais Mwai Kibaki alikuwa rais wa tatu wa taifa la Kenya kati ya mwaka 2002 hadi 2012.