Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja akamatwa

Muhtasari

•Sakaja alikamatwa Ijumaa alasiri na kupelekwa katika makao yao makuu ya DCI yaliyo Kiambu Road, Nairobi.

•Mapema Ijumaa Sakaja alimkashifu Kinoti kufuatia ripoti hiyo na kumdhubutu achukue hatua ya kumkamata.

Johnson Sakaja
Johnson Sakaja
Image: Ezekiel Aming'a, KWA HISANI

Seneta wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja ametiwa mbaroni.

Sakaja alikamatwa Ijumaa alasiri na kupelekwa katika makao yao makuu ya DCI yaliyoko Kiambu Road, Nairobi.

Mmoja wa mawakili wake, Kamotho Adrian,  amesema seneta huyo alikamatwa na maafisa wanne wa DCI kutoka ofisi yake huko Riverside ambapo alikuwa amemaliza mkutano wa kampeni na wajumbe kutoka jamii ya Wakamba.

Timu ya mawakili ilidai kuwa wamenyimwa idhini ya kuingia makao makuu ya DCI, wakidai maafisa hao waliwaambia wanapaswa kupata kibali kutoka ‘juu’.

“Ndiyo, amekamatwa kutoka Riverside na tuko nje ya langi baada ya kunyimwa nafasi ya kuandamana na mteja wetu. Wanachukua mkondo wa kisiasa kupita kiasi,” Kamotho aliambia Star.

Akielezea wasiwasi wake, wakili huyo alisema maafisa hao wa DCI hawakuwahi kueleza ni kwa nini walikuwa wakimkamata Sakaja.

"Popote walipo na mteja wetu(Sakaja), hawawezi kumhoji bila kuwepo kwa mawakili wake, kwa hivyo tunasubiri maafisa wa DCI watupe fursa," Kamotho aliongeza.

Habari za kukamatwa kwa seneta huyo zilitangazwa kwanza na mtaalamu wa masuala ya kidijitali Dennis Itumbi.

"Sakaja Johnson akamatwa, yupo katika makao makuu ya DCI,"  Itumbi alitangaza kupitia Twitter.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya gazeti la Nation kuripoti kwamba DCI Kinoti alimtaja Sakaja kama mshukiwa wa uhalifu wa kimataifa ambaye wanachunguza.

Katika ripoti hiyo, Kinoti pia amenukuliwa akisema DCI haitasalimisha jiji kuu kwa ulaghai na kwamba watahusisha mashirika yote ya kimataifa katika kuchunguza na kushtaki yeyote aliyehusika katika udanganyifu wa masomo.

Mapema Ijumaa Sakaja alimkashifu Kinoti kufuatia ripoti hiyo na kumdhubutu achukue hatua ya kumkamata.

"Vitisho vya kukamatwa na kuteswa na serikali havitatutisha wala kubadili nia ya watu wa Nairobi. Azimio letu linabaki thabiti. Bwana DCI Kinoti, niko ofisini kwangu Riverside, karibu au nijulishe kama ungependa nije," Sakaja alisema Ijumaa asubuhi kupitia Facebook.

Sakaja anawania kuwa gavana wa  Nairobi kwa tikiti ya UDA. Aliidhinishwa na IEBC kuwania kiti hicho mnamo Juni 7, 2022.

Siku mbili baadaye, malalamishi manne yaliwasilishwa kutaka kibali chake kifutiliwe mbali kwa madai kuwa Shahada yake ya Sayansi ya Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Timu ya Uganda ni ya kughushi.

Mengine yanafuata...