Bei ya unga wa mahindi kupungua kwa shilingi 2

Kulingana na taarifa iliyosambazwa, muungano wa wasaga nafaka umekubali kupunguza bei ya unga kwa shilingi 2 serikali ikiondoa tozo za uagizaji.

Muhtasari

• Waziri wa Kilimo Peter Munya aliahidi wasaga nafaka kwamba kuanzia Julai mosi, serikali itasitisha tozo zote za uagizaji nafaka.

• Hilo litarahisisha wasaga nafaka kuagiza bidhaa hiyo na kuifikisha kwa mwananchi katika bei ya kumudu.

Unga wa mahindi kwenye duka la jumla
Image: The Star

Ni afueni kwa Wakenya baada ya uvumi wa taarifa kwamba muungano wa wasaga nafaka nchini Kenya kuafikia makubaliano ya kupunguza bei ya unga wa mahindi nchini.

Muungano huo ulitoa taarifa hii siku mbili tu baada ya Waziri wa Kilimo, Peter Munya kuahidi kwamba serikali itasitisha tozo zote zinazotolewa kwa uaguzaji wa bidhaa ya nafaka kutoka mataifa ya nje.

Ila muungan huo ulitilia shaka tamko hilo kwa kusema kwamba kuondoa tozo zote hakutakuwa na athari chanya kwa kiasi kikubwa kwa watumizi wa bidhaa ya unga wa ugali kwani hilo litasababisha kupunguzwa kwa bei ya mfuko wa kilo mbili ya unga wa ugali kwa shilingi mbili peke yake.

Waziri Peter Munya juzi akizungumza katika kaunti ya Kajiado alisema kwamba serikali itachapisha agizo la kuondolewa kwa tozo hizo ili wasaga nafaka hao wawe na afueni katika kuagiza mahindi na nafaka kutoka mataifa ya nje kama njia moja ya kupunguza bei ya unga ambayo imepanda kwa kasi mno katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Waziri huyo alisema kwamba mfumuko wa bei ya unga wa ugali ni kutokana na tozo kama hizo ambazo serikali inatoza kwa nafaka inayoagizwa kutoka nje, jambo ambalo limefanya nafaka kuwa ghali kwa mkenya wa kawaida.

“Tumeamua kwamba serikali itatoa tozo zote zinazolimbikizwa kwa mahindi yanayoagizwa kutoka nje kwa muda wa siku tisini. Kuanzia Julai mosi, hakuna ada itakayotozwa kwa mahindi yaliyoagizwa kutoka nje,” alitoa ahadi Waziri Peter Munya.

Akionekana kutoa ushauri kwa serikali, Waziri Munya alisema kwamba ni wakati sasa serikali ya Kenya ifungue njia za mawasiliano za moja kwa moja na mataifa ambako nafaka huagizwa kama vile Tanzania na majirani wake Zambia na Malawi ambako nafaka imekuwa ikiagizwa kutoka huko na wasaga nafaka nchini.

Mawasiliano hayo yataleta tija kwani serikali itashawishi mataifa hayo kuondoa vibali vya kuuza nje pamoja na tozo zingine ili kufanya rahisi bidhaa hiyo kuagizwa.

Kwa sasa, bei ya mfuko wa kilo mbili za unga wa mahindi imefumuka kutoka kati ya shilingi 90-100 miezi michache iliyopita hadi shilingi kati ya 210-220.