Chuo kikuu cha Moi kimetangaza kufuta kazi wafanyakazi kadhaa

Barua iliyosambazwa mitandaoni inasema chuo hicho kimefikia uamuzi wa kusimamisha watu kazi kutokana na changamoto za kifedha.

Muhtasari

• Chuo hicho kilitoa sababu kuwa ni ongezeko la deni la mishahara huku mapato ya chuo yakizidi kudidimia.

Chuo Kikuu cha Moi - Eldoret
Image: Mathews Ndanyi (The Star)

Uongozi wa chuo kikuu cha Moi kilichopo mjini Eldoret umetoa taarifa zisizo za kufurahisha kwa wafanyakazi wake baada ya kutoa barua inayowataarifu kuhusu vibarua vya baadhi yao kuota nyasi hivi karibuni.

Katika barua hiyo ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii inayoaminika kutoka katika chuo hicho, uongozi unasema kwamba chuo hicho hakina uwezo wa kukimu baadhi ya mahitaji kutokana na ongezeko la deni na pia kupungua kwa mapato ya chuo hicho.

Kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya wafanyakazi katika chuo hicho wamefahamishwa kuwa tayari kukanyaga lami.

Image: Twitter

Barua hiyo iliyotiwa Saini ya naibu chansela wa chuo hicho profesa Isaac Kosgey, inaeleza kwamba tatizo la ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli za chuo hicho halijaanza leo na kusema kwamba chuo hicho kimekuwa kikikumbana na tatizo hilo kwa miaka mingi sasa.

“Kama mnavyojua, chuo hiki kimekuwa kikikumbana na changamoto ya kuafikia wajibu wa malipo ya mishahara. Kwa miaka mingi sasa deni la mishahara limekuwa likiongezeka, ambalo kwa sasa linachukua hadi asilimia 70 ya mtaji wetu kutoka kwa hazina ya chuo,” sehemu ya barua hiyo ilitaarifu.

Naibu chansela alisema katika barua hiyo kwamba kutokana na ongezeko kubwa la deni la mishahara na kupungua kwa mapato ya chuo, imekuwa vigumu kwa shughuli nyingi kuendelea kawaida chuoni humo.

“Chuo kimeshindwa kuendelea na ongezeko hili la deni la mishahara na hivyo tumeamua kuchukua hatua Madhubuti ili kupunguza idadi ya huduma za watu tunaofanya nao kazi ili kuhakikisha shughuli za chuo hazilemazwi,” barua hiyo ilizidi kusema.

Barua hiyo ilisisitiza kwamba hilo ndilo linapelekea chuo kufanya kuwa lazima, kupunguza idadi ya wafanyakazi na kuwataarifu wafanyikazi wote kuwa tayari maana shoka la hukumu huenda linadondoshwa vichwani mwao muda wowote.

Hii inatokea wakati ambapo Wakenya wengi wanazidi kuteta kuhusu mzigo mzito wa ugumu wa maisha ambao wametwishwa vichwani kutokana na hali ya uchumi kuzorota nchini, ikisemekana chanzo ni vita vya Urusi na Ukraine.