"Hata Mimi Nataka Kujua Nini Kilimuua Kijana Yule," - Didmus Barasa baada ya Kukamatwa

Alisema hata yeye ako tayari kujuzwa nini kilitokea kwa dereva Brian Olunga ambaye anatuhumiwa kumuua

Muhtasari

• Barasa alisema alikuwa ameelekea Nairobi kupata dhamana alipoona taarifa kwa runinga za kumtaka ajisalimishe kwa polisi.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa
Image: FACEBOOK//DIDMUS BARASA

Baada ya mbunge wa Kimilili Didmus Barasa kujisalimisha mapema Ijumaa kufuatia amri ya kitengo cha upelelezi wa jinai, sasa mbunge huyo ameonekana kujitenga na tuhuma zinazomuandama kuhusu kifo cha dereva wa mshindani wake ambaye anatuhumiwa kumuua papo hapo kwa kumpiga risasi kichwani usiku wa Jumanne Agosti 9.

Akionekana kujitenga na kifo chake, Barasa sasa anadai kwamab kama mtu yeyote yule pia na yeye anataka kujua ni kilichomuua dereva Brian Olunga ambaye alikuwa dereva wa mshindani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha Kimilili, Brian Khaemba kutoka chama cha DAP-K.

Akizungumza na vyombo vya habari punde baada ya taarifa kusambaa kwamba amejisalimisha kwa vyombo vya dola, mbunge huyo alisema anashirikiana na polisi wakati wanachunguza suala hilo na kusema kwamba hakuwa amekimbilia nchi Jirani ya Uganda kama ambavyo fununu zilisema.

“Nilikwenda Nairobi kupata dhamana tarajiwa nikisubiri kukamatwa lakini nilipoona kwenye runinga kamanda wa polisi wa mkoa akinitaka nijisalimishe, niliendesha gari hadi eneo hili na niko tayari kutoa ushirikiano kwa polisi ili pia nijue nini kilimuua kijana huyo,” Barasa alisema.

Mbunge huyo alidai kuwa siku ya Jumapili, mmoja wa walinzi wake alivamiwa na kujeruhiwa vibaya na kwa sasa yuko hospitalini akiendelea kupata nafuu.

Barasa alisema pia alishambuliwa siku hiyo hiyo na kuripoti kisa hicho kwa polisi.

“Kulikuwa na watu wengine waliokuwa na bunduki akiwemo mshindani wangu, afisa wa polisi aliyekuwa anasimamia vituo vya kupigia kura. Pia tutakuwa tukitoa maombi kwamba silaha zote zilizokuwepo zifanyiwe uchunguzi wa kitaalamu,” alisema.

Mbunge huyo alijiwasilisha katika kituo cha polisi cha Bungoma na kuwekwa chini ya ulinzi huku uchunguzi wa kesi ya mauaji ukiendelea.

Siku ya Alhamisi, polisi walimpa makataa ya saa sita kujisalimisha kwa kituo chochote cha polisi, siku moja tu baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Noordin Haji kutoa kibali cha kukamatwa kwake baada ya kusemekana kuenda mafichoni baada ya kitendo hicho cha mauaji.