Mahakama yaidhinisha kifungo cha miaka 67 cha Mbunge John Waluke

Mahakama ilisema mashtaka dhidi ya Waluke na Wakhungu yalithibitishwa bila shaka yoyote.

Muhtasari

•"Adhabu hazikuwa kubwa zaidi. Zipo ndani ya sheria. Hatia na hukumu zimethibitishwa," alisema Jaji.

•Wawili hao waliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni na Sh20 milioni mtawalia mnamo Septemba 2020 baada ya kukaa jela kwa miezi mitatu.

John Waluke
John Waluke
Image: Tony Wafula, KWA HISANI

Mahakama kuu imeidhinisha kifungo cha miaka 67 cha Mbunge wa Sirisia John Waluke kuhusiana na kesi ya bodi ya nafaka na mazao (NCPB) inayohusisha Shilingi milioni 313.

Jaji Esther Maina alisema mashtaka dhidi ya Waluke na Grace Wakhungu yaliyokuwa mbele ya Hakimu Elizabeth Juma yalithibitishwa bila shaka yoyote.

"Adhabu hazikuwa kubwa zaidi. Zipo ndani ya sheria. Hatia na hukumu zimethibitishwa," alisema Jaji.

Maina alisema Waluke na Wakhungu watalazimika kulipa faini au kutumikia vifungo hivyo.

Wakhungu kwa upande wake alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 69 gerezani.

Iwapo hawatalipa faini zilizowekwa na mahakama ya mwanzo ambayo ni zaidi ya shilingi  Bilioni mbili, watalazimika kutumikia kifungo cha muda mrefu gerezani.

Wawili hao waliachiliwa kwa dhamana ya Shilingi 10 milioni na  milioni 20 mtawalia mnamo Septemba 2020 baada ya kukaa jela kwa miezi mitatu.

Walifungwa Juni 22, 2020 na Mahakama ya Kupambana na Ufisadi baada ya kupatikana na hatia ya ulaghai na kujipatia  Sh297 milioni kinyume cha sheria kupitia mikataba ya ukora katika Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Wawili hao wanaweza kukata rufaa katika mahakama ya rufaa.