Ofisi za UDA kaunti ya Siaya zateketezwa na waandamanaji

Ofisi hizo zinadaiwa kuchomwa na kundi la vijana wanaoshiriki katika maandamano.

Muhtasari

• Uteketezaji huu unakuja wiki moja baada ya ofisi za UDA Kisumu kuchomwa.

Ofisi za UDA kaunti ya Siaya
Ofisi za UDA kaunti ya Siaya
Image: Faith Matete

Makao makuu ya chana cha UDA katika kaunti ya Siaya yametiwa moto na halaiki yenye ghadhabu ambao wameitikia wito wa maandamano ya Alhamisi kutoka kwa kinara wa upinzani Raila Odinga.

Katika picha na video ambazo zimeenezwa mitandaoni adhuhuri ya Alhamisi, ofisi hizo za chama tawala zinaonekana zikiteketea, am,bapo inaarifiwa kwamba ni kundi la vijana wanaoegemea mrengo wa Azimio waliotekeleza uteketezaji huo.

Aidha, haijabainika iwapo kuna uvamizi na wizi wa mali uliofanyika kabla ya kuteketezwa.

Haya yanakuja takribani wiki mbili baada ya ofisi zingine za UDA kaunti ya Kisumu kuporwa mali kabla ya kuharibiwa vibaya na kundi la vijana wanaoshiriki katika maandamano.

Katika uharibifu huo, pia gari moja lililokuwa nje ya ofisi hizo Kisumu liliteketezwa.

Uharibifu huo unafanyika wakati ambapo kinara wa Azimio na viongozi wengine wa muungano huo wakiwa katika msafara wa kuongoza maandamano jijini Nairobi, maeneo ya Imara Daima.