Waombolezaji 6 wahofiwa kufariki katika ajali ya Kendu Bay

Baadhi ya waombolezaji pia wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Muhtasari

•Basi la Shule ya Sekondari ya ACK Guu lilikuwa likiwasafirisha waombolezaji kuelekea mazishi katika wadi ya Karachuonyo Magharibi.

•Shahidi Kenneth Abila alisema lori hilo lilikuwa limetoka barabara ya Kanyadhiang -Pala.

lililohusika katika ajali ya barabarani Mei 5, 2023.
Basi la Shule ya Sekondari ya ACK Guu lililohusika katika ajali ya barabarani Mei 5, 2023.
Image: ROBERT OMOLLO

Takriban watu sita wanahofiwa kufariki baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani karibu na Kanyadhiang, eneo bunge la Karachuonyo.

Ajali hiyo ya Ijumaa ilitokea wakati basi la Shule ya Sekondari ya ACK Guu lilikuwa likiwasafirisha waombolezaji kuelekea mazishi katika wadi ya Karachuonyo Magharibi.

Basi hilo lilipinduka wakati dereva akijaribu kukwepa kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa likija na mwendo kasi.

Wakaazi walisema dereva alipoteza udhibiti wa basi hilo alipokuwa akikwepa lori katika makutano ya Kanyadhiang. Ajali ilitokea kando ya barabara ya Kanyadhiang-Pala wakati basi hilo lilikuwa likipitia kona kutoka barabara ya Kendu Bay -Homa Bay.

Shahidi Kenneth Abila alisema lori hilo lilikuwa limetoka barabara ya Kanyadhiang -Pala.

“Baadhi ya waombolezaji pia wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini... Lori lilikuwa likienda kwa kasi," Abila alisema.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kaskazini Lydia Parteyie alithibitisha kisa hicho akisema basi hilo liliondoka barabarani kabla ya kutua kwenye mtaro.