Basi la Chuo Kikuu cha Moi lililokuwa likielekea Mombasa lahusika katika ajali ya barabarani

Basi hilo ambalo lilikuwa limebeba wanafunzi 50 lilianguka katika eneo la Limuru, kaunti ya Kiambu.

Muhtasari

•Naibu kamanda wa polisi wa Lari, Francis Njomo alisema wanafunzi 12 walikimbizwa katika hospitali ya Orthodox katika mji wa Kimende.

•Alisema kuwa dereva wa basi hilo alishindwa kulidhibiti katika mazingira yasiyoeleweka na basi likatua kwenye mtaro.

wa Chuo Kikuu cha Moi walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini
Wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu cha Moi walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini
Image: GEORGE MURAGE

Basi la Chuo Kikuu cha Moi, lililokuwa likielekea Mombasa limehusika katika ajali ya barabarani katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Basi hilo ambalo lilikuwa  limebeba wanafunzi hamsini lilianguka katika eneo la Kimende katika kaunti ndogo ya Lari, kaunti ya Kiambu.

Kwa bahati nzuri, wanafunzi wote waliokuwemo wako salama, taasisi hiyo imethibitisha.

"Wanafunzi wote wako salama. Tunashukuru," Chuo hicho kilisema.

Wanafunzi kumi na wawili hata hivyo walipata majeraha madogo.

Naibu kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Lari, Francis Njomo alisema wanafunzi hao walikimbizwa katika hospitali ya Orthodox katika mji wa Kimende.

Njomo alithibitisha kuwa basi hilo lilikuwa na wanafunzi 50.

Aliongeza kuwa dereva wa basi hilo alishindwa kulidhibiti katika mazingira yasiyoeleweka na basi likatua kwenye mtaro.

Njomo alisema polisi wa trafiki wameanzisha uchunguzi kubaini kilichotokea kabla ya ajali hiyo.

"Tunachunguza ili kubaini jinsi dereva alivyopoteza udhibiti na basi hilo kushuka barabarani," alisema.

Hata hivyo, shahidi aliyeshuhudia, John Kimani alisema dereva wa basi hilo alikuwa akijaribu kutoroka gari lingine lililokuwa likiendeshwa vibaya.

Kimani amewataka madereva kuendesha magari kwa uangalifu haswa katika maeneo ya Kimende, Uplands, Magina, Kinale na viunga kwa kuwa eneo hilo linafunikwa na ukungu nyakati za asubuhi jioni.

"Hakuna mtu anayehitaji kuzidisha mwendo, hali ya hewa ni ya baridi sana. Barabara ni utelezi na huwezi kuona umbali ambao mtu anatakiwa kuuona anapoendesha," Kimani aliongeza.

Njomo alisema mabaki ya basi la chuo hicho kikuu yalivutwa hadi kituo cha polisi cha Lari huku uchunguzi ukiendelea.