logo

NOW ON AIR

Listen in Live

El Nino Kenya: idadi ya waliofariki yafikia 61 huku familia 80,518 zikiathirika

Serikali ya kaunti na ya kitaifa inawaomba wakaazi kuzingatia onyo na kuondoka katika maeneo hatari.

image
na Davis Ojiambo

Habari20 November 2023 - 06:22

Muhtasari


  • • Idadi ya waliofariki kutokana na mvua hiyo sasa imefikia 61, huku watu 235 wameripotiwa kujeruhiwa na wengine wanane wameorodheshwa kama hawajulikani walipo.
  • • Serikali  inasema kuwa  mvua ya El Nino sasa imeathiri kaunti 33, kutoka 19 za mwanzo.
Picha inayoashiria jinsi mvua za El Nino zinavyoendelea kuathiri maeneo mbalimbali nchini

Mvua za El Nino zinazidi kuwaathiri watu wengi nchini Kenya huku taarifa kutoka kwa idara za hali ya anga zikisema mvua hizo zitazidi kushuhudiwa kwa siku kadhaa zijazo.

Wakiwa katika makundi, wakaazi wa Kaunti ya Tana River wako kwenye harakati wakitafuta eneo la juu zaidi lililo salama, ambalo liko mbali na maeneo yaliyofurika ambayo yamefagia nyumba zao, mali zao na mifugo yao.

Si kazi rahisi au nafuu kwa watu ambao sasa wanayumbayumba kutokana na athari mbaya za mvua za El Nino.

Wakazi wa kijiji cha Bondi wanahofu kuwa maji yanaongezeka kwa kasi katika makazi yao na hivyo wanawake, watoto wanaume kufanya safari hiyo ya kujikinga huku wakiiomba serikali iwasaidie makazi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Wakaazi hao ni miongoni mwa maelfu ya familia ambazo zimeathiriwa na mvua zinazoendelea za El Nino. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema tangu mvua kuanza kunyesha Oktoba, familia 80,518 zimeathirika, huku karibu nusu ya idadi hiyo zikihama.

Biashara, vituo vya afya, na shule pia zimeathirika huku mvua zikiendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.

Idadi ya waliofariki kutokana na mvua hiyo sasa imefikia 61, huku watu 235 wameripotiwa kujeruhiwa na wengine wanane wameorodheshwa kama hawajulikani walipo.

Miongoni mwa walioripotiwa kutoweka ni wafanyikazi wawili wa kukusanya ushuru KRA ambao gari lao lilisombwa katika eneo la Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale walipokuwa wakisafiri kuelekea Mombasa.

Wakati huo huo, serikali  inasema kuwa  mvua ya El Nino sasa imeathiri kaunti 33, kutoka 19 za mwanzo.

Hakika, maeneo ya kaskazini mwa Kenya yanaendelea kupata athari mbaya zaidi za mvua. Huko Wajir, miji yote imezama, shule, vituo vya afya na vituo vya polisi vimekosa ukarimu na maisha kuhatarishwa na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua.

Ili  kuepukana  na hasara zaidi, serikali ya kaunti na ya kitaifa inawaomba wakaazi kuzingatia onyo na kuondoka katika maeneo hatari.

Serikali ya kitaifa kupitia afisi ya naibu rais inaendelea kutoa wito kwa hatua madhubuti kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuziba njia za maji, kuhamia maeneo ya miinuko, na kaunti kutoa pesa kusaidia kupunguza athari za El Nino.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema serikali ya kitaifa inajitahidi kupeleka helikopta kuwaokoa waliokwama na kuratibu misaada kwa wanaohitaji msaada wa kibinadamu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved