Tazama safari ya mapenzi ya Zari na Shakib, watafanya harusi rasmi Oktoba 3

Walikutana mara ya kwanza 2019, wakachumbiana kwa muda kabla ya kutengana kisha kurudiana mwaka jana.

Muhtasari

•Zari na mchumba wake Shakib wanatarajiwa kufunga pingu za maisha katika harusi rasmi ya kizungu mnamo Oktoba 3.

•Walihalalisha muungano wao kwa mara ya kwanza katika harusi ya kidini ya Kiislamu (Nikah) mapema mwaka huu.

Safari ya mapenzi ya Zari na Shakib.

Wapenzi mashuhuri wa Uganda, Zarinah Hassan na Shakib Cham Lutaaya wanatarajiwa kufunga pingu za maisha katika harusi rasmi ya kizungu hivi karibuni.

Barua ya mwaliko ambayo ilifikia Radio Jambo inaonyesha kuwa harusi hiyo itafanyika Jumanne, Oktoba 3 mwendo wa saa sita adhuhuri.

“Zarinah Hassan na Shakib Lutaaya wanakualika kwa moyo mkunjufu kushiriki katika furaha na kusherehekea siku yao ya harusi. Tarehe: 3 Oktoba 2023. Saa: 1200. Uwepo wako kwenye siku hii maalum utafanya sherehe yetu isisahaulike.” ilisomeka barua ya mwaliko ambayo ilitiwa saini na Zari na Shakib.

Harusi itakayofanyika nchini Afrika Kusini itahudhuriwa na wageni wachache tu ambao wamealikwa na maelezo mengi kuihusu yamewekwa faragha. 

Wawili hao walihalalisha muungano wao wa muda mrefu kwa mara ya kwanza katika harusi ya kidini ya Kiislamu (Nikah) mapema mwaka huu.