•Stephen Orengo alinusurika kifo Alhamisi jioni wakati polisi walimuokoa kutoka kwa umati wenye hasira wa wanafunzi waliokuwa wakitaka kumuangamiza.
•Tukio hilo linaaminika lilitokana na mzozo wa mapenzi kwani wawili hao wanasemekana kuwahi kuwa kwenye mahusiano.
Inasikitisha! Kijana asafiri kutoka mbali kumuua mpenziwe kwa kisu kufuatia mzozo wa mapenzi
Polisi katika kaunti ya Kisii wanamzuilia kijana mmoja anayedaiwa kumuua mwanafunzi wa chuo cha Kisii National Polytechnic, anayesemekana kuwa mpenzi wake wa zamani.
Stephen Orengo alinusurika kifo siku ya Alhamisi jioni wakati polisi walipomuokoa kutoka kwa umati wenye hasira wa wanafunzi waliokuwa wakitaka kumuangamiza kwa madai ya kumuua Lucy Boke ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.
Mshukiwa huyo anayeripotiwa kutoka eneo la Kuria Magharibi anasemekana kumfuata msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 hadi nyumbani kwakekatika mtaa wa Jogoo Estate, mjini Kisii siku ya Alhamisi usiku na kumuua ndani ya nyumba yake. Inasemekana alisafiri umbali mrefu kutoka nyumbani kwao Kaunti ya Migori hadi Kisii kutekeleza uhalifu kwa tuhuma za ukosefu wa uaminifu katika mahusiano.
Rafiki wa marehemu alisema kuwa Orengo aliwafuata nyuma walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka shuleni kabla ya marehemu kumbainishia wazi kuwa hataki uhusiano wowote naye.
Majirani waliosikia kilio cha marehemu hawakuweza kuokoa maisha yake wakati wa tukio hilo la kuhuzunisha na mwili wake uliokuwa umejeruhiwa vibaya ulipatikana ndani ya chumba chake. Kulikuwa na dalili za mapambano na madoa ya damu ndani ya nyumba hiyo, ikiashiria kwamba marehemu alijaribu kupigania maisha yake kabla ya Orengo kufanikiwa kumdunga kisu mara kadhaa na kusababisha kifo chake cha uchungu.
Kulingana na watu wa karibu, tukio hilo linaaminika lilitokana na masuala ya uhusiano kwani wawili hao wanasemekana kuwa wapenzi wa zamani.
Maafisa wa upelelezi waliofika katika eneo la uhalifu walifanikiwa kupata kisu cha jikoni ambacho kilitumiwa kumuua mwanafunzi huyowa chuo kikuu.
"Ninatoa wito kwa vijana wetu kwamba kila mara wanapogundua kuwa wana migogoro, wasitumie njia yoyote ya vurugu katika kutatua masuala yao," mkuu wa polisi wa Kisii Central, Isaac Kimwele alisema.
Baadaye mshukiwa alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Kisii Central huku mwili wa marehemu Lucy Boke ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kisii Teaching and Refferal.