Uchaguzi Uganda

Idadi ya waliofariki katika maandamano Uganda yafikia 7

Hadi kufikia sasa aidi ya watu 40 wamejeruhiwa

Muhtasari

 

  •  Maelfu ya watu wanafurika barabarani kulalamikia kukamatwa kwa Bobi Wine
  • Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.

 

Na BBC

Watu saba wamefariki dunia nchini Uganda kufuatia maandamano yaliyofanyika jana Jumatano ya kupinga kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Msemaji ameiambia BBC kuwa zaidi ya waandamanaji 40 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo na polisi.

Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda limesema kuwa wafanyakazi wake waliwasaidia watu 11 waliokuwa na majeraha ya kupigwa risasi.

Wakati huohuo, Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine atakapoachiwa huru.

Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.

 Bobi Wine alikamatwa jana Jumatano, Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.

Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru.

Taarifa ya polisi haikusema watu hao wamefariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki dunia.

Polisi pia imesitisha matukio kadhaa ya kampeni ya wagombea wa upinzani.

Mawakili wa Bobi Wine wanasema bado mteja wao hajafikishwa mahakamani.

Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia alikamatwa na kuachiwa huru.

Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.

Marekani imeshutumu ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Ujumbe wa Marekani umesema kuwa "pande zote zipinge vita" na kuchukua hatua za kupunguza hofu iliyotanda nchini humo.

Bobi Wine alikamatwa wakati wa mkutano wa kampeni kwa madai ya kukiuka miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliyowekwa na Tume ya uchanguzi.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye wafuasi wake walianza maandamano wakidai aachiliwe huru.

Uganda itafanya uchaguzi wa urais mnamo mwezi Januari 2021.