Kesi ya Murunga: Mpenzi wa kando aruhusiwa kuchukuwa DNA

Muhtasari

• Agnes Wangui  amedai kupata watoto wawili na marehemu mbunge huyo.

• Wangui na wanawe wawili wameruhusiwa kuhudhuria mazishi yake na kushirikishwa katika mipango ya mazishi.

Aliyekuwa mbunge wa Matungu marehemu Julius Murunga. (Picha: HISANI)
Aliyekuwa mbunge wa Matungu marehemu Julius Murunga. (Picha: HISANI)

Hakimu Peter Muholi siku ya Ijumaa aliruhusu kuchukuliwa kwa sampuli za DNA kutoka kwa mwili wa aliyekuwa mbunge wa Matungu Justus Murunga.

Hii ni baada ya mwanamke aliyedai kuwa ‘mpango wake wa kando’ Agnes Wangui  kudai kupata watoto wawili na marehemu mbunge huyo.

Agizo hilo la hakimu Muholi linafuatia ombi la kila upande kutoa mwanapatholojia wa kibinafsi kwa gharama zao wenyewe kutekeleza shughuli hiyo.

 

Mwili wa marehemu utaruhusiwa kuchukuliwa kwa mazishi siku ya Jumamosi au siku yoyote ile ambayo familia itaafikiana kumzika.

Wangui na wanawe wawili wameruhusiwa kuhudhuria mazishi yake na kushirikishwa katika mipango ya mazishi.

Siku ya Jumatatu, Wangui alidai kwamba Murunga alikuwa na mipango ya kuishi naye na wanawe wawili mtaani Karen.

Alisema kwamba marehemu alikuwa tayari amenunua kipande cha ardhi mtaani Karen mjini Nairobi na mipango ya ujenzi wa nyumba ilikuwa imeanza.

“Murunga pia alikuwa ametaka kuhalalisha uhusiano wetu kabla ya kufahamisha familia yake au umma. Alikuwa ametaka ndoa yetu ifanyike kuambatana na tamaduni za jamii ya Agikuyu. Kwa bahati mbaya kifo kimetupokonya Murunga kabla ya kutimiza azimio lake,” Wangui alisema.