Kitanzi! mfungwa wa shambulizi la Chuo kikuu cha Garissa ajinyonga

Mohammed Abdi, Hassan Edin Hassan na raia wa Tanzania Rashid Charles Mberesero wakiwa katika mahakama ya Milimani Juni 19, 2019. Picha : AKELLO ODENYO
Mohammed Abdi, Hassan Edin Hassan na raia wa Tanzania Rashid Charles Mberesero wakiwa katika mahakama ya Milimani Juni 19, 2019. Picha : AKELLO ODENYO

Mfungwa aliyekuwa anatumikia kifungo cha maisha katika gereza la Kamiti baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki shambulizi la kigaidi katika chuo kikuu cha Garissa amepatikana akiwa amefariki.

Polisi na maafisa wa magereza walisema kwamba Rashid Mberesero, mwenye umri wa miaka 26 alijitia kitanzi akitumia kitambaa cha blanketi lake katika seli yake iliyoko Block H.

Mwili wa raia huyo wa Tanzania ulipatikana ukining’inia kwa dirisha na kitambaa cha blanketi shingoni mwake.

Maafisa walisema kisa hicho kilifanyika mwendo wa saa tisa alasiri siku ya Ijumaa baada ya wafungwa kupata chakula cha mwisho cha siku. Mwili wake ulipelekwa kwa chumba cha kuhifadhi maiti cha City.

Mberesero alikuwa amewasilisha rufaa dhidi ya hukumu yake na kesi yake ilikuwa inasubiri kusikizwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Marehemu alikuwa mnamo Julai 3, 2019 na wenzake wawili amehukumiwa kuhusiana na shambulizi la kigaidi katika chuo kikuu cha Garissa mwaka 2015 ambapo watu 148 waliuawa.

Wenzake, Hassan Edin na Mohamed Abdi wote raia wa Kenya walifungwa miaka 41 gerezani kila mmoja na bado wako gerezani.

Watatu hao walikuwa wamepatikana na hatia ya kushirikiana kutekeleza shambulizi la kigaidi na kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Mberesero alipewa hukumu kali kuliko wenzake kwa sababu alikamatwa katika eneo la tukio na alishindwa kueleza alichokuwa akifanya katika eneo hilo. 

Aprili 2, 2015 dunia iligutushwa na shambulizi baya zaidi la kigaidi kuwahi kutokea katika himaya ya Kenya. Wanamgambo wa Al Shabaab walikuwa wamevamia chuo kikuu cha Garissa na kuua wanafunzi 148.

Washambulizi hao pia waliacha watu 83 na majeraha mabaya huku familia nyingi zikiachwa na makovu ya shambulizi hilo milele.