Aliyekuwa mbunge Anthony Mutahi ashtakiwa kwa unyakuzi wa ardhi

Muhtasari

  • Anadaiwa kuiba hati miliki ya ardhi yenye thamani ya Shilingi milioni 18.5.

  • Alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Martha Mutuku.

Mbunge wa zamani Anthony Kimaru kizimbani, alishtakiwa kwa kughushi stakabadhi za ununuzi wa ardhi.
Mbunge wa zamani Anthony Kimaru kizimbani, alishtakiwa kwa kughushi stakabadhi za ununuzi wa ardhi.

Mbunge wa zamani wa Laikipia Mashariki Anthony Mutahi Kimaru alishtakiwa siku Alhamisi asubuhi kwa kuiba hati miliki ya ardhi yenye thamani ya Shilingi milioni 18.5.

Kimaru alishtakiwa kwa kuiba hati miliki ya kipande cha ardhi chenye nambari ya usajili LR. 10422/13 Mjini Nanyuki inayomilikiwa na George Odinga na David Mortons Silverstein ambao ni wasimamizi wa marehemu Livia Lepoer Trench.

Alidaiwa kutenda kosa hilo mnamo Agosti 5,2016 katika makao makuu ya wizara ya ardhi mjini Nairobi.

Kimaru pia alikabiliwa na shtaka lingine la kughushi stabadhi ya makubaliano kwa kipande cha ardhi LR. 10422/13 Nanyuki tarehe 3 Agosti, 2009 na kudanganya kwamba ni halali na ilitolewa na Mwangi Kariuki advocates.

Korti iliambiwa kwamba Kimaru pia alitaja kuwepo kwa makubaliano ya uuzaji kwa Silas Kimeli ambaye ni naibu Msajili wa mahakama kuu ya Nyeri.

Alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu wa Milimani Martha Mutuku na aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Shilingi laki tatu au dhamana ya Shilingi milioni moja na mdhamini.

Kesi hiyo itatajwa Januari 28.