Uganda yapinga madai ya Museveni kupewa kisiri chanjo ya corona

Muhtasari
  • Uganda yapinga madai ya Museveni kupewa kisiri chanjo ya corona
  • Kufikia sasa Uganda imethibitisha kuwa na wagonjwa 40,221 wa corona
  • Katika ujumbe wa Twitter, Wizara ya Afya imesema hakuna aliyepewa chanjo kati ya rais na wandani wake wa karibu kama ilivyodaiwa
Museveni
Rais Yoweri Museveni Museveni

Waziri wa Afya wa Uganda, Jane Aceng, amekanusha ripoti zinazoashiria kwamba maafisa wa ngazi ya juu serikalini wamepewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kabla ya nchi kupokea rasmi chanjo hiyo.

Bi. Aceng alikuwa akijibu taarifa zilizochapishwa katika gazeti la Daily Monitor nchini humo na gazeti la Marekani la Wall Street Journal.

Katika ujumbe wa Twitter, Wizara ya Afya imesema hakuna aliyepewa chanjo kati ya rais na wandani wake wa karibu kama ilivyodaiwa.

"Ninataka kusema waziwazi kwamba Rais Museveni na maafisa wake wakuu hawajachanjwa dhidi ya Covid-19," waziri alisema.

Kufikia sasa Uganda imethibitisha kuwa na wagonjwa 40,221 wa corona.

Nchi hiyo inatarajia kupokea msaaada wa dozi 100,000 za chanjo aina ya AstraZeneca kutoka India na dozi zingine 300,000 za chanjo ya Sinopharm kutoka China.

Haijabainika ni lini chanjo hizo zitawasili nchini humo.