Kanisa katoliki Tanzania lataka tahadhari zaidi zichukuliwe Dhidi ya corona

Muhtasari
  • Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Katoliki nchini Tanzania (TEC) limewataka wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona
  • Dkt Kitima pia amesisitiza kutegemea sala pekee hakutaweza kuondosha tatizo hilo nchini humo
Image: AFP

Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Katoliki nchini Tanzania (TEC) limewataka wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona.

Katibu wa TEC Padri Charles Kitima hii leo kupitia mkutano na wanahabari amesisitiza kuwa tishio la corona bado lipo Tanzania na Kanisa na ongezeko la vifo bado linaendelea kuripotiwa ikiwemo ndani ya Kanisa lenyewe

''Ndani ya miezi iliyopita Mapadri 25 wamepoteza maisha kwa matatizo ya kupumua. Masisita na manesi zaidi ya 60. Vifo vinaendelea, tuchukue tahadhari."

 

Kwa mujibu wa Dkt Kitima japo serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa waraka wa kuwataka watu kuchukua tahadhari bado kuna changamoto kwa kuwa watu hawabanwi kisheria kuchukua tahadhari.

''Changamoto tuipatayo kwa kuwa serikali haijasisitiza tahadhari, watu bado wana mtazamo kuwa corona haipo au imeisha kama ilivyokuwa mwaka jana."

Dkt Kitima pia amesisitiza kutegemea sala pekee hakutaweza kuondosha tatizo hilo nchini humo.

'' Mungu si hirizi, anataka binadamu tuwajibike. Corona ipo, unaambiwa chukua tahadhari unasema ushasali...Mungu wetu anataka tuwajibike , tutende majukumu yetu kwa karama na utashi tuliopewa."

Baraza la Maaskofu pia limetaka taarifa rasmi zitolewe kuhusu ugonjwa huo pamoja na kufanyika kwa tafiti juu ya ugonjwa huo na wanasayansi wa ndani.

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu Kanisa Katoliki nchini Tanzania kutoa tamko juu ya ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo.

Tamko la kwanza lilitolewa kwa njia ya waraka mwezi Januari ambapo Raisi wa TEC Askofu Gervaas Nyaisonga alitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona.

 

Katika waraka huo kanisa lilisitiza Tanzania si kisiwa na kutaka tahadhari zote za kisayansi kuchukuliwa.

Tahadhari hii ya Kanisa katoliki inatolewa huku Shirika la afya duniani (WHO), likiendelea pia kuitaka Tanzania kuchukua hatua zaidi kukabiliana na Covid-19.